Tambwe ajitamba hazarani asema mashabiki wasubiri mabao zaidi yanakuja


 

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, ndiye gumzo hivi sasa katika soka la Tanzania baada ya mabao yake mawili kuipa timu yake ushindi wa 2-0 dhidi ya BDF XI lakini kitu kikubwa ni kwamba, muda mfupi tu baada ya kuwaua Wabotswana hao, klabu yake imempatia nyumba.
Tambwe alifanikiwa kufunga mabao hayo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wakati mashabiki wakitoka uwanjani walikuwa wakiimba: Tambwe, Tambwe, Tambwe…”
Mrundi huyo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita (alipachika mabao 19), aliachwa na Simba katika usajili wa Desemba, mwaka jana na juzi ndiyo alianza kuwaonyesha Yanga kwamba yeye ni nani katika suala la kuzifumania nyavu kutokana na mabao yake kuwapa ushindi.
Mabao hayo aliyofunga Tambwe, yamesababisha aweke rekodi ya kufunga mabao yote manne msimu huu kwa kutumia kichwa.Bao lake la kwanza msimu huu alilifunga akiwa na Simba kwenye mzunguko wa kwanza katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Emmanuel Okwi dakika ya 36.
Bao lake la pili alilifunga akiwa na Yanga katika mzunguko wa pili kwenye sare tena ya mabao 2-2 dhidi ya Azam baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Telela, kabla ya juzi kuweka tena kambani mabao mawili kwa vichwa katika mchezo dhidi ya BDF dakika ya kwanza na ya 55, akiunganisha krosi za Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Tambwe alisema amefurahi kufikisha mabao matatu akiwa na Yanga lakini akatamba kwamba ataendelea kufunga zaidi kama Mungu akiendelea kumpa afya.
“Naamini nitaendelea kufanya vizuri zaidi. Hiyo ndiyo kiu yangu kubwa, nataka niwape furaha mashabiki wa Yanga.“Mungu anazidi kuwaonyesha Simba kwamba walikuwa wanafiki kwa tuhuma walizokuwa wakinipatia,” alisema Tambwe.
“Tangu nijiunge na Yanga nilikuwa nikijisikia vibaya kwa sababu nilikuwa sifungi hali hiyo pia ilinifanya nijione ni mwenye deni kubwa sana kwa klabu yangu hii ambayo hakika naweza kusema inanijali sana.
“Hata hivyo namshuru sana Mungu kwa kusikia kilio changu na kunifanya niisaidie timu yangu kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, hakika nimefarijika sana na najiona kama nimezaliwa upya.
“Nawashukuru pia wachezaji wenzangu wote kwa ushirikiano wao mkubwa wanaouonyesha kwangu, siku zote na katika mechi ya leo (juzi).” Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga nao umemzawadia Tambwe zawadi ya nyumba mpya ya kuishi kwa kipindi chote atakachokuwa akiitumikia klabu hiyo kutokana na kuwezesha kuibuka na ushindi dhidi ya BDF XI.
Nyumba hiyo ipo Sinza Mori jijini Dar es Salaam na nyota huyo ambaye kwa sasa anaiishi Mabibo jijini hapa, anatarajia kuhamia Jumatano hii.
Share on Google Plus

0 comments: