Simba dume lao.

 


KOCHA wa Simba, Goran Kopunovic, jana aliamua kuonyesha jeuri kwa mashabiki wa Yanga baada ya kuwaambia ‘tulieni-tulieni’ kisha kuwaonyesha ishara ya kuwataka wakae kimya, kauli ambayo aliitoa wakati timu yake ilipopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Moro.
Simba imeifunga Polisi Moro katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kufufua matumaini ya kufanya vizuri katika ligi hiyo ambapo sasa imefikisha pointi 20 ikiwa imepaa kutoka nafasi ya tisa hadi ya tatu. Pointi hizo ni tano nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Azam FC.
Ikicheza kwa kujiamini na kuonyesha soka safi, Simba ilipata mabao hayo katika kila kipindi ambapo wafungaji walikuwa ni Ibrahim Ajibu na Elius Maguri.
Mchezo mgumu kwa Polisi
Ajibu aliipatia Simba bao la kwanza kwa kichwa katika dakika ya 14 akiunganisha krosi nzuri ya beki wake, Juuko Murshid.  Maguri alifunga bao la pili katika dakika ya 63 baada ya uzembe wa mabeki wa Polisi wakati wakiokoa.
Kopunovic azomewa, Aveva ajificha
Mara baada ya kuingia uwanjani, mashabiki ambao wanadhaniwa kuwa ni wa Yanga, walianza kumzomea Kopunovic huku wakitoa maneno ya vijembe kutokana na mwenendo wa timu yake kusuasua katika ligi hiyo. Kocha huyo hakujibu kitu.Rais wa Simba, Evans Aveva, baada ya kuona zomeazomea inaongezeka, hakutoka kwenye gari aliloingia nalo uwanjani hapo mpaka mwisho wa mchezo.
Lakini dakika tano kabla ya mechi kumalizika wakati Simba ikiongoza mabao 2-0, Kopunovic aliwageukia mashabiki waliokuwa wakimzomea na kuwaambia ‘tulieni-tulieni’, kisha akawaonyesha ishara ya kuwataka wakae kimya na hapohapo akawageukia wale wa Simba na kujikuta akipata shangwe za nguvu.
Ivo Mapunda akimbizwa hospitali
Kipa wa Simba, Ivo Mapunda aliumia kwa kuchanika juu ya jicho baada ya kutokea piga nikupige langoni kwake, ambapo alipatiwa huduma ya kwanza uwanjani kisha akaondolewa uwanjani kwa gari la wagonjwa kwa ajili ya matibabu zaidi huku nafasi yake ikichukuliwa na Peter Manyika.
Simba Ukawa wapigwa
Wakati mechi ikiendelea, kuna baadhi ya mashabiki wa Simba Ukawa walionekana wakiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni hirizi, baada ya kuona hivyo mashabiki wengine wa Simba walianza kupigana nao hao mashabiki kiasi cha kupelekana nje ya uwanja.
Sababu kubwa ya ugomvi wao huo ni madai kuwa wale waliokutwa na hirizi walikuwa wakizuia ushindi wa Simba, baadhi ya wale waliofanyiwa fujo na kupigwa hawakurejea tena ndani ya uwanja baada ya kutolewa.
 
Makocha wafunguka
Kocha wa Polisi Moro, Adolf Rishard, alikiri kuwa timu yake haikucheza vizuri na wachezaji wake hawakuwa makini lakini akawataka kutokatishwa tamaa na matokeo hayo. Upande wa Kopunovic alisema uwanja haukuwa na ubora mzuri na uliharibu mipango yake mingi lakini akawataka mashabiki kuendelea kuwaunga mkono.
Share on Google Plus

0 comments: