OKWI AINGIA MITINI KAMBI YANGA



Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi ameanza vituko Yanga baada ya kuondoka kikosini na kushindwa kuambatana na wenzake walioingia kambini jana Bagamoyo, Pwani.
Wachezaji 20  wa Yanga  waliingia kambini kujiandaa na mechi ya Jumapili  Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Ruvu,  itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van Der Pluijm aliliambia gazeti hili jana kuwa hakuambatana na Okwi kwa vile hakuwapo kambini wakati timu yake inajiandaa na safari ya Bagamoyo.
“Okwi hayupo kambini na hakuna anayejua sababu za kutokuwapo kwake, lakini niseme kwamba ni makosa, ingawa hilo naliacha kwa uongozi utajua nini cha kufanya,” alisema Pluijm.
Mdachi huyo amekuwa akiwalalamikia washambuliaji wakiongozwa na Okwi, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na Jerry Tegete kwa kiasi kikubwa kuwa wamekuwa chanzo cha timu hiyo kufanya vibaya kwa sababu ya kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazopata kufunga mabao katika baadhi ya mechi.
“Katika eneo ambalo linaumiza kichwa ni la ushambuliaji, nina washambuliaji wengi wazuri  pengine kuliko timu yoyote kwenye ligi, lakini hawafanyi ambacho wanatakiwa kufanya, wanapata nafasi nyingi lakini hawazitumii na hivyo kuikosesha timu ushindi.
Akizungumzia madai hayo, Kavumbagu amesisitiza kuwa wachezaji wenzake na wapenzi wa klabu hiyo, waache kutafutana uchawi na badala yake wapambane kwa ajili ya kutetea taji kwa sababu bado nafasi ipo.
Mshambuliaji huyo alisema: “Wanaosema tunacheza chini ya kiwango siyo kweli kama mechi yetu na Mgambo JKT aliyekuwapo alishuhudia  jinsi tulivyojitolea, lakini mazingira ya mchezo yalikuwa magumu na hali ya uwanja haikuwa nzuri.”
Mbali ya Okwi, Pluijm aliwataja wachezaji wengine ambao hawakuingia kambini jana kuwa ni viungo Haruna Niyonzima na Athumani Idd ‘Chuji’.
Kocha huyo alisema wachezaji hao hakuwajumuisha kwa sababu ni wagonjwa, hivyo amewapa muda wa kupumzika.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga, umepinga madai ya kuwa unawachunguza nyota wake, Juma Kaseja na Kelvin Yondani kwa madai  ya kuhujumu mechi yao dhidi ya Mgambo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema hakuna ukweli kuhusu yanayosemwa kuhusu mchezo huo na yaliyotokea ni sehemu ya makosa ya kawaida ya mchezo.
Share on Google Plus

0 comments: