CCM WACHEMKA KWENYE MAPENDEKEZO YA KAMATI BUNGENI

1


Mapendekezo ya CCM ya kutaka kufanya marekebisho katika baadhi ya vifungu katika Ibara ya 1 ya Rasimu ya Katiba yamegonga mwamba baada ya kukosa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar.
Hali hiyo imejitokeza katika kamati tatu kati ya 12 ambazo zimeanza kutoa matokeo ya kura baada ya mjadala.
Wakitoa taarifa kwa waandishi wa habari, mwenyeviti wa Kamati Namba 1, Ummy Mwalimu na Namba 10, Anna Abdallah, walisema kuwa theluthi mbili imekosekana katika baadhi ya vifungu kwenye ibara hiyo.
Walisema kwamba vipengele vilivyokosa theluthi mbili ya kura zilizopigwa, vitapelekwa bungeni pamoja na hoja zilizotolewa na wengi na wachache. Abdallah alisema ibara nyingi walizozipigia kura katika kamati yake hazikupata theluthi mbili ya kura.
“Kwa mfano muundo wa serikali kwa vyovyote vile hatupati theluthi mbili, ila tunapata walio wengi wanataka nini. Walio wengi wanataka mfumo wa serikali mbili, kwa hiyo taarifa yetu itakuwa na maoni ya wajumbe wengi, na ile wachache,” alisema Anna.
Alikiri kuna wajumbe wachache ambao wanataka muundo wa shirikisho la serikali tatu, lakini hawawezi kusema hao ndio wameshinda.
Alitolea mfano wa ibara ya pili ya sura ya kwanza ambayo inazungumzia mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo waliafikiana kuongeza milima na anga.
Alisema kuwa ibara hiyo ilikubaliwa na wajumbe wote baada ya kuongezwa maeneo hayo mawili.
“Maeneo yenye utata ikiwamo kwenye muundo wa serikali ndio tumeshindwa kupata theluthi mbili ya kura zilizopigwa na wajumbe kutoka pande mbili za Muungano,” alisema.
Naye  Mwalimu alisema ibara ya 1 katika sura ya kwanza hawakupata theluthi mbili pande zote mbili.
Alisema uamuzi huo si wa mwisho, bado watakwenda katika Bunge la Katiba kupigiwa kura za jumla.
Pamoja na kamati nyingine kuendelea kupiga kura, habari za ndani zinasema upatikanaji wa theluthi mbili katika ibara hiyo ya kwanza umekuwa mgumu.
Share on Google Plus

0 comments: