TIMU YA JAJI WARIOBA YATUPIWA VIRAGO NJEE

 

Tumeisoma kwa umakini mkubwa taarifa iliyotolewa juzi na Ikulu, ikikanusha madai ya mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kwamba Ikulu imeitupia virago Tume hiyo. Tumejaribu kuisoma taarifa hiyo ya Ikulu tena na tena, aya kwa aya, mstari kwa mstari na neno kwa neno. Lakini kadiri tulivyozidi kufanya hivyo ndivyo tulivyozidi kugundua kuwa ni dhahiri Tume hiyo, siyo tu ilitupiwa virago, bali pia ilidhalilishwa na kufadhaishwa kutokana na lugha ya kejeli na masimango iliyokuwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.
Jaji Warioba alikaririwa akilalamikia jinsi yeye na makamishna wa Tume walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari kwa namna ambayo iliwadhalilisha, kwani licha ya hatua hiyo kuchukuliwa kwa haraka bila kusubiri siku ambayo Tume ilikuwa imepanga kufanya makabidhiano, Serikali haikutaka kujipa muda wa kufanya maandalizi ya kuwarudisha wajumbe makwao.
Katika kuhalalisha hatua hiyo ya Serikali, taarifa ya Ikulu ilijikita zaidi katika kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinachoelekeza kwamba shughuli za Tume zingekoma rasmi baada ya mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge la Katiba. Ikulu ilisema katika taarifa hiyo kwamba Jaji Warioba aliwasilisha Rasimu hiyo bungeni Machi 18 na siku iliyofuata Rais alitia saini tangazo la kuvunja Tume hiyo kwa mujibu wa sheria, hivyo ilishangazwa na kitendo cha mtu “kujitia amesahau siku hiyo kwani hicho ni kiwango cha juu sana cha unafiki”.
Hata hivyo, jambo linalomtatiza Jaji Warioba na wenzake ni uharaka wa Serikali kuivunja Tume hiyo wakati ikijua kwamba Tume ilikuwa haijamaliza kazi yake wakati ilipokabidhi Rasimu hiyo kwa Rais. Jaji Warioba anasema Serikali ilikuwa ikijua kwamba Tume ilikuwa ikiendelea na kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita la Rasimu pamoja na maelezo aliyoyatoa wakati wa kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge la Katiba.
Lakini pia Jaji Warioba anasema kuwa hata kama sheria ilitaja muda wa kuvunja Tume hiyo, bado Serikali ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha inavunjwa katika mazingira yanayokubalika kama zilivyovunjwa tume zote zilizotangulia, kwani sheria hiyo haikuzuia kufanya hivyo.
Sisi tunadhani kuwa kwa kuzingatia utamaduni uliozoeleka, Tume ingevunjwa rasmi katika mazingira ya kistaarabu na heshima kama tulivyoshuhudia ikizinduliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Ikulu, Aprili 13, 2012.
Tunashindwa kuelewa kiini cha udhalilishaji huo mkubwa kwa Tume hiyo, pamoja na Rais Kikwete kuimiminia sifa na pongezi nyingi kwa kuweka utaifa mbele. Akipokea Rasimu hiyo Desemba 31, 2013 katika viwanja vya Ikulu, Rais Kikwete alisema Tume hiyo imefanya kazi iliyotukuka na ya kihistoria na kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu waige mfano wake pindi Bunge hilo litakapoanza kazi ya kujadili Rasimu na hatimaye kuandika Katiba mpya. Sasa nini kimetokea kiasi cha Tume hiyo kuonekana kama imefanya uhaini ni kitendawili ambacho hakijateguliwa.
Sisi tunadhani kwamba haikuwa sahihi kwa Serikali kuwadhalilisha Jaji Warioba na makamishna wa Tume hiyo, hata kama pengine haikufurahishwa na baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba waliyoiwasilisha.
Kwa kuzingatia kwamba Tume hiyo iliundwa na watu ambao uzalendo wao hauwezi kutiliwa chembe ya shaka, Serikali ilipaswa kuienzi kazi waliyofanya hata kama kwa shingo upande.
Share on Google Plus

0 comments: