TANESCO; MATRILIONI KUMALIZA MGAWO WA UMEME NCHINI

Wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka na wakati mwingine kupata hasira kutokana na kutopata umeme wa uhakika tangu miaka ya 1980. Wakati mwingine wanapata hasira baada ya vyombo vyao kuungua kwa mfano, friji, redio na televisheni kutokana na umeme kukatika na kurejea kwa kasi .
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) sasa, halipendi tena wateja wake wateseke kwa kuingia gizani kwa muda wa siku tatu, saa mbili mpaka saa 12, na pia hawataki tena kuwapo kwa ahadi hewa, bali sasa wanataka mapinduzi ya umeme wa uhakika kuanzia mijini mpaka vijini.
Kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme kila siku nchini na kuwapo kwa umeme mdogo, sasa Tanesco inaboresha miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam, kufunga mfumo mpya wa umeme katika Kanda ya Kaskazini Mashariki kutoka Dar es Salaam, Chalinze, Segera Tanga, Kilimanjaro mpaka Arusha.
“Mradi huu utakuwa ni wa kilometa 682 ambao utakamilika mwaka 2016 baada ya kugharimu Sh616 bilioni, tunataka wananchi wapate umeme wa uhakika,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba.
Tanesco vilevile inatarajia kuunganisha umeme kutoka Nairobi nchini Kenya, kupitia Arusha, mpaka Mbeya, mradi ambao utagharimu Sh433 bilioni.
Katika mchakato wa mradi huu, Tanzania ipo tayari kuanza, lakini upande wa Kenya inasita kuanza kwa mradi kutokana na sababu mbalimbali.
Pia Tanesco inakusudia kutekeleza mradi mwingine mkubwa katika Kanda ya Kaskazini Magharibi, inayojumuisha Mkoa wa Mbeya, Sumbawanga, hadi Kigoma kwenye eneo la Nyakanali na kuunganisha njia za umeme ambazo zinatokea Kahama.
Mramba anasema gharama za umeme kwenye kanda hiyo ni Sh960 bilioni na unatarajiwa kukamilika mwaka 2017 katika umbali wa kilometa 660. Mradi mwingine utaunganisha njia za umeme kutoka Geita mpaka Nyakanazi, mkoani Kigoma ambao utagharimu Sh35 bilioni.
Pia Tanesco imejipanga kufunga nyaya za umeme kutoka jijini Dar es Salaam mpaka mkoani Mtwara, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kunakuwapo umeme wa uhakika endapo mradi wa umeme wa gesi utakuwa na hitilafu.
“Tutakuwa na mradi mwingine wa umeme wa kilometa 650 kutoka mkoani Mtwara mpaka Songea. Mradi huo utagharimu Sh640 bilioni, utakuwa kilometa 650 na utakamilika mwaka 2015,” anabainisha mkurugenzi huyo.
Uboreshaji mkubwa Dar es Salaam
Katika Jiji la Dar es Salaam moja ya miradi mikubwa ya kukabiliana na mgao wa umeme ni kufunga nyaya za umeme, kukarabati vituo 13 vya umeme kati ya 20 na kujenga vituo zaidi ya saba vipya vidogo vya vyenye uwezo wa 33kv mpaka 11kv. Vituo vipya vitajengwa Mwananyamala, Jangwani Beach, Kigogo, Tegeta, Muhimbili, Luguruni, na Mikocheni. Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, miradi hiyo tayari imeanza kutekelezwa.
Share on Google Plus

0 comments: