HUU NDIO UKUBWA WA TATIZO LA KUKOSA CHOO

Waswahili wanao usemi maarufu kuwa, raha ya nyumba ni choo.Kwa hakika, hawakukosea kwani chakula chochote kinapoliwa lazima kitumike mwilini na mabaki yake kutolewa kwa njia ya haja kubwa.
Hata hivyo, binadamu wa  jinsi zote, umri au rika baadhi yao wanakabiliwa na tatizo la kukosa choo, ambalo linawasumbua kweli. Tatizo hilo ambalo huzaa au kuambatana na tatizo jingine la kupata choo kigumu linatesa.
Kwa kawaida, mtu anapopata tatizo hili hutumia muda wake mwingi chooni akijaribu kusukuma haja kubwa wakati mwingine bila mafanikio.
Ni dakika chache zinazohitajika kumaliza haja inapotoka kwa urahisi, lakini kwa wenye tatizo hilo, dakika hizo hazitoshi kwao kumaliza haja.
Ugumu wa kuitoa haja hiyo huwasababishia maumivu makali na pengine kuzalisha maradhi mengine.
Kwa mtu anayeishi kwenye nyumba ya kupanga na yenye wapangaji  wengi wanaotegemea chumba kimoja cha choo zikiwamo zile za mijini, mmoja wao anapokuwa na tatizo hili la kupata choo kigumu  inaweza kuwa kero kwa wenzake.
Kwa ufupi,  mtu anapoingia chooni kujisaidia, wenzake hukaa nje wakisubiri kwa muda zamu zao za kuingia…hakika huwa ni mateso kwake na kero kwa wapangaji wenzake.
Tatizo la kukosa choo (constipation)
Kukosa choo kwa siku moja kitaalamu,  siyo tatizo, isipokuwa mtu anaweza kutajwa kuwa na tatizo hilo iwapo atakosa choo kwa angalau zaidi ya saa 72, yaani siku tatu.
Akizungumzia tatizo hili,  Mtaalamu wa Viungo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) , Dk Raymond Mwonekano anasema kwa kawaida kila mtu anatakiwa apate choo angalau mara tatu kwa wiki. “Kama mtu atakosa choo kwa siku tatu mfululizo, atahesabika kuwa na tatizo, lakini lazima awe amekula chakula kwa siku zote hizo.
Mtu ambaye hajala hawezi kuhesabika kuwa na ugonjwa huo bali atakuwa na tatizo jingine,” anasema.
Anaongeza kuwa tatizo hilo linatokana na haja kubwa kwenda taratibu na hivyo kuchelewa kutoka kwa wakati mwafaka.
Share on Google Plus

0 comments: