BUNGE LA KATIBA LAPINGWA KUENDESHA MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA



Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Mwalimu Nyerere Idealogy Conservation Society ya jijini Tanga, imefungua Kesi Mahakama Kuu ikitaka kuzuia mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Taasisi hiyo inapinga mchakato huo wa Katiba kwa kile inachodai kuwa ni kasoro zilizojitokeza, ikiwamo wananchi kukosa uwakilishi uliotokana na ridhaa yao, posho kubwa wanayolipwa wajumbe na gharama kubwa zilizotumika katika maandalizi ya Bunge hilo.
Kesi hiyo ya madai namba 02/2014, ilifunguliwa Februari 17, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Muzzammil Mussa Kalokola.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa kwa stakabadhi ya malipo ya Serikali namba 49803745, ni Waziri wa Sheria na Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), (kwa sasa ni Frederick Werema) na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
Hata hivyo Jaji Werema na Jaji Warioba wamesema hawana taarifa za kesi hiyo.
Dk. Kalokola alisema katika hati yake ya madai kuwa anataka mchakato huo wa Katiba usitishwe kwa kuwa umevunja Katiba iliyopo.
Amesema Katiba ya sasa imekiukwa katika Muundo wa Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika utekelezaji wa majukumu na wajibu wake wa kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Madadiliko ya Katiba ibara ya 98.
“Vilevile imeshindwa kuzingatia hadidu za rejea kama zilivyoainishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83,” alisema Dk Kalokola.
Dk. Kalokola alifafanua kuwa Katiba ya sasa imeweka masharti kadhaa, ikiwamo utaratibu wa namna ya kuibadilisha na sheria nyingine ambazo zimeanishwa katika ibara ya 98 na Sheria ya mwaka 1984 Na.15 ib.14.
“Ibara ya 98 (1) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni zifuatazo,” alisema huku akiinukuu ibara hiyo na kuendelea:
“Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote.
“Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.”
Share on Google Plus

0 comments: