ZAIDI YA MASAA MANNE YATUMIKA KUTENGANISHA MAPACHA WALIOKUWA WAMEUNGANA MUHIMBILI

 
Jopo la Madaktari Bingwa Saba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa ya hospitali hiyo (Moi), wamefanikiwa kuwatenganisha pacha waliokuwa wameungana kiwiliwili.
Iliwalazimu mabingwa hao kutumia saa nne kufanikisha upasuaji huo. Mmoja wa watoto hao waliotenganishwa, amelazwa kwenye Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU) Taasisi ya Mifupa Moi wakati kiwiliwili kingine kilifariki.
Jopo la madaktari waliofanikisha upasuaji huo ni; bingwa mstaafu wa watoto ambaye aliitwa maalumu kwa kazi hiyo, Petronila Ngiloi, Dk Robert Mhina (mifupa) na Profesa Karim Manji aliyekuwa akifuatilia kwa karibu mapigo ya moyo.
Wengine ni Dk Karima Khalid aliyekuwa akiratibu dawa ya usingizi, Dk Hamis Shaaban (ubongo na uti wa mgongo), Dk Zaitun Bokhary (bingwa upasuaji watoto) na Dk Nyangasa (moyo na mishipa ya fahamu).
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Dk Shaaban alisema walimfanyia vipimo mtoto ambaye hakuwa amekamilika na kugundulika kuwa hakuwa amekamilika viungo vyote achilia mbali kutokuwa na kichwa na macho pia hakuwa na moyo, figo, tumbo, maini ila alikuwa na uti wa mgongo.
“Uti wa mgongo ulikuwepo na ndio uliokuwa umeshikana na mwenzake na kuna mshipa mmoja wa fahamu ulikuwa unafanya kazi ndio maana alikuwa ukimgusa anachezesha mguu.”
Alisema kinachoratibiwa kwa sasa ni kuangalia dawa ya usingizi aliyopewa mtoto ambaye anaendelea kupumua na kwamba ndani ya saa 24, dawa ya usingizi waliyomuwekea mtoto huyo itakuwa imeisha na ataanza kunyonya kama kawaida
Share on Google Plus

0 comments: