KASEJA SASA KULA SHAVU NDANI YA FC LUPOPO JAMHURI YA KIDEMOCRASIA YA KONGO

DAU alilotengewa Golikipa namba moja wa timu ya Taifa, Juma Kaseja na klabu ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni zaidi ya ada ya uhamisho waliyotumia TP Mazembe kumsajili Mbwana Samatta, kutoka klabu ya Simba mwaka 2011, ambayo ilikuwa dola 150,000 (sawa na Sh milioni 225).

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa Lupopo Balanga Ismael alisema, Kaseja, atajiunga rasmi na FC Lupopo, mara baada ya kumaliza
majukumu yake na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, ambayo inaingia kambini leo kujiandaa na mechi ya mwisho ya mchujo ya kuwania kushiriki Kombe la Dunia, mwakani nchini Brazil, mchezo utakaochezwa Septemba 7 Banjul, Gambia.

Balanga alisema wamefanikisha mazungumzo ya kumsajili kipa huyo na kilichobakia ni Kaseja kwenda Congo na kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo mapema mwezi ujao, huku akishindwa kutaja dau hilo ni kiasi gani.

“Jana (juzi) tulimpelekea mkataba tulioutafsiri kwa Kiingereza, baada ya ule wa awali uliokuwa kwa Kifaransa, ameridhia vyote vilivyokuwa kwenye mkataba na tumekubali matakwa yake, ambapo pia alikuwa akipokea ushauri kutoka kwa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ambao walikuwa wakimsimamia.

“Tulitaka kuondoka naye leo (jana) kwenda Congo, ili akasaini mkataba huo, lakini TFF walituambia ana majukumu ya timu ya Taifa, kujiandaa na mchezo wa Gambia, hivyo baada ya majukumu ya timu ya taifa ataondoka moja kwa moja kuelekea Congo kusaini mkataba na kujiunga nasi,” alisema Ismael.

Aidha Balanga alisema jina la Kaseja ni la kwanza kwenye orodha yao ya wachezaji, waliowapeleka katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Congo DRC (FECOFA), kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi ya Congo, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 11 mwaka huu.
Share on Google Plus

0 comments: