WANAUME WATAKIWA KUFUNGA UZAZI IWAPO WANAISI WAMEPATA WATOTO WAKUTOSHA

 
Ni nadra kwa wanaume kukubali kufunga uzazi, lakini waliofanya hivyo wameona mafanikio yake.
Sumbawanga. “Baada ya kupata mtoto wa nne nilidhani mke wangu asingeweza tena kushika mimba kutokana na umri aliokuwa nao, lakini nilishangaa baada ya kukaa miaka kumi akapata ujauzito na ndipo nilipoamua kwenda kufunga uzazi,”anasema Bevin Mtendo (55).
Mtendo, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa amekuwa kivutio kikubwa kwenye jamii tangu alipoamua kufunga uzazi mwaka 2008 kutokana na wanaume wengi kumfuata kuomba ushauri.
Anasema ana watoto watano na kwamba mtoto wa mwisho alimpata baada ya miaka kumi baada ya kudhani kuwa mke wake asingeweza kuzaa tena.
Anasema kabla ya kufunga uzazi, mke wake alikuwa akitumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, lakini baada ya kujifungua mtoto wa nne aliacha na kudhani kuwa hawezi kupata tena ujauzito.
Hata hivyo, anasema baada ya miaka kumi kupita mkewe alipata ujauzito hali iliyomlazimu yeye kuamua afunge uzazi.
“Tulijua hatuwezi kupata tena mtoto, lakini alipokuja huyu wa tano
niliona sasa bora mimi nikafunge na nilipomwambia mke wangu alifurahi,”anasema.
Mtendo anasema alishauriwa na rafiki yake ambaye naye alifunga baada ya kupata watoto wanane.
“Mwanzoni watu wengi walinishangaa na kudhani siwezi kufurahia tena tendo la ndoa, lakini siyo kweli nafurahia vizuri tena situmii muda mrefu na nikihitaji huduma hiyo napewa,”anasema na kuongeza:
“Kama unahisi umepata watoto wa kutosha, njia nzuri ni kufunga na kama unataka kuamini gonga gogo usikie mlio wake,”anasema.
Kwa kawaida operesheni ndogo kwa ajili ya kufunga uzazi huchukua kati ya dakika 15 hadi 20, lakini Mtendo anasema kwake yeye ilimchukua dakika 45 kwa sababu aliyemfanyia alikuwa hajatoa huduma hiyo kwa muda mrefu.
Kuhusu dhana kwamba mwanamume aliyefunga uzazi anakuwa siyo rijali tena, Mtendo anajibu: “Siyo kweli kabisa tena urijali unaongezeka na hata mke wangu sasa hivi anafurahi zaidi kwa sababu awali kabla sijafanyiwa nilikuwa natumia muda mfupi, lakini sasa hivi natumia muda mrefu kidogo na kuna siku huwa namshinda.”
Share on Google Plus

0 comments: