WAANDISHI WAPINGA CHADEMA KUJENGA MNARA WA MWANGOSI

CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoani Iringa (IPC), kimepinga ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Nyololo kwenye eneo alilofia Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho Daudi Mwangosi unaotakiwa kutekelezwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mwenyekiti wa IPC, Frank Leonard alisema Chadema wameazimia kujenga mnara huo bila kuwashirikisha waandishi wa habari jambo ambalo kamwe halitaunga mkono.

Alisema IPC haiungi mkono suala hilo kwa vile Mwangosi alikuwa kazini alipopatwa na maafa hayo.

Leonard amesema si vema siasa ikaingia kwenye kumbukumbu za kifo cha kiongozi wao.

“Msimamo wetu kama chama kutokana na bodi yetu tunapinga asilimia 100 azimio la Chadema kujenga mnara wa mwandishi mwenzetu bila kutushirikisha.

“Sisi kama chama hatujaafiki hilo kwa sababu kazi wanayofanya ilitakiwa ifanywe na waandishi wa habari hivyo ilitakiwa tuwaalike sisi na siyo wao watualike,”alisema.

Alisema Chadema wanaamini kuwa marehemu Mwangosi alikuwa mkereketwa wao ingawa wanahabari hawaamani jambo hilo.

Leonard alisema ni hatari kutumia
jina la Mwangosi kwa malengo ya siasa.

Alisema iwapo Chadema wanataka kujenga mnara wa kuwaenzi watu wanaopata maafa katika mikutano waanzie Arusha na Morogoro ambako maafa kama hayo yalitokea.

Katibu wa IPC, Francis Godwin alisema: “Kuanzia sasa waandishi habari tunaruhusiwa kufanya kazi na polisi kwa vile na Kamanda wa Polisi, Michael Kamuhanda aliyehusisha na kifo cha Mwandosi amekwisha kuhama”.

Daudi Mwangosi aliuawa Septemba 2 mwaka jana akiwa kwenye ufunguzi wa tawi la Chadema huko Nyololo wilayani Mufindi.
Share on Google Plus

0 comments: