ULINZI SHIRIKISHI WATUMIKA KUTAPELI KITUO KIKUU CHA MABASI UBUNGO

 
Hali ya usalama kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (UBT), imekuwa tete baada ya kuibuka kwa kundi kubwa la matapeli wanaowaibia abiria na kuwabambikizia kesi kwa kutumia njia ya ulinzi shirikishi.
Mbali na kufanyika kwa vitendo hivyo kituo hicho kinadaiwa kuwa soko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya Bangi na Mirungi.
Kundi hilo ambalo linajulikana kama vishoka limekuwa likifanya vitendo hivyo kuanzia saa mbili usiku kwa kujifanya kuwa wao ulinzi shirikishi, na kufanya utapeli huo kwa kuwakamata abiria na baadhi ya watu wanaoingia kwenye kituo hicho na kuwapa makosa mbalimbali.
Uchunguzi uliyofanywa na gazeti hili takriban siku tatu kwenye kituo hicho majira usiku na mchana, umebaini kwamba mchezo huo mchafu umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu ambapo tayari kundi kubwa la watu wametapeliwa na kuibiwa vitu mbalimbali.
Uchunguzi huo umebaini kwamba moja ya utapeli unaofanywa na kundi hilo la vijana wanaojiita ulinzi shirikishi, ni kutumia pete feki za dhahabu ambazo wanazitumia kuwatapeli fedha abiria.
Pia, licha ya kufanya utapeli huo kwa kutumia dhahabu feki, kundi hilo linatumia bidhaa ya sabuni kuwatapeli simu abiria. Sabuni hutengenezwa kwa mfano wa simu na kuwabambika watu kuwa ni simu halisi.
Licha ya kufanyika kwa vitendo hivyo, uchunguzi pia umebaini kuwepo
kwa biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Uchunguzi pia umebaini kwamba vijana hao matapeli wakimkamata mtu kwa kisingizio cha kuhusika na wizi, wanamtoza faini kati ya Sh50,000 hadi 70,000. Makosa yanayodaiwa kuwa madogo kama kukojoa au kutupa uchafu wanatoza faini ya kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 kila siku.
Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo (NHC), Amani Sizia alithibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo vya uhalifu na kudai kwamba UBT imegeuka kuwa shamba la bibi kwa wahalifu.
Sizia alisema: “Kwa kweli hali ya kituo cha mabasi ya Ubungo na maeneo jirani imekuwa mbaya sana, kuna vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo ni feki zaidi ya vitano. Vikundi hivyo vimekuwa vikifanya kazi ya kuwatapeli abiria.”
Alisema kwa kuthibitisha zaidi nyakati za usiku kila kibaka anageuka kuwa mlinzi shirikishi, na kufanya kazi ya utapeli ili kujipatia fedha.
“Nashukuru sana ndugu yangu mwandishi kwa kunitafuta UBT kwa sasa haifai, kuna vitendo vingi vya uhalifu ambavyo vinafanyika nyakati za usiku. Kila kibaka ikifika wakati huo anageuka kuwa mlinzi shirikishi,” alisema Sizia
Share on Google Plus

0 comments: