Kwa mara nyingine, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemshauri Spika wa Bunge, Anne Makinda kubadili uamuzi wake na kuzirejesha kamati za Bunge za Mashirika ya Umma (POAC) na Hesabu za Serikali (PAC), akisema ilikuwa sio sahihi kuziunganisha kamati hizo kama alivyofanya.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mapema mwaka huu,
Spika Makinda aliifuta POAC na kuunganisha shughuli zake na Kamati ya
PAC, hatua ambayo kiongozi huyo wa CAG anasema ilikuwa ni makosa kwa
sababu uamuzi huo usingeleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya ofisi
yake ya kudhibiti na kukagua fedha za umma. Wakati Spika Makinda
alipochukua hatua hiyo, CAG huyo alionyesha wasiwasi wake hadharani na
kusema ungekuwa muujiza mkubwa iwapo
hatua hiyo ya Spika ingeongeza tija na ufanisi katika ofisi yake.
hatua hiyo ya Spika ingeongeza tija na ufanisi katika ofisi yake.
Hoja ya CAG wakati huo ilikuwa kwamba shughuli za
kamati hizo zilikuwa nyingi mno kiasi cha wajumbe wa kamati hizo
kulemewa, kwa maana ya kushindwa kupata muda wa kutosha kufuatilia kwa
umakini utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huduma za kijamii pamoja na
kuhakiki matumizi ya fedha katika Serikali Kuu na mashirika ya umma kwa
mujibu wa Ripoti ya kila mwaka ya CAG ya ukaguzi wa hesabu za taasisi
hizo za umma.
Sasa baada ya miezi kadhaa tangu Spika Makinda
achukue hatua hiyo, CAG amelazimika tena kutoa kauli ya kumshauri ili
afikirie upya uamuzi wake wa awali. Bila shaka CAG amefikia hatua hiyo
baada ya kufanya tathmini jadidi na kujiridhisha kwamba mabadiliko
aliyoyafanya Spika yamedhoofisha shughuli za kudhibiti na kukagua
matumizi ya fedha za umma badala ya kuongeza tija na ufanisi.
Anachosema CAG ni kuwa, hata kabla ya kamati hizo
kuunganishwa, Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC), ilikuwa tayari
ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kusimamia zaidi ya mashirika 128 ya
umma nchini, hivyo hatua ya Spika kuiunganisha na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), ambayo ina wakala, wizara na idara mbalimbali ni
kuibebesha mzigo usiobebeka.
Mengi yalisemwa wakati huo na hakika mengine mengi
yameendelea kusemwa kuhusu nini hasa lilikuwa lengo la Spika katika
kuchukua hatua hiyo yenye utata mkubwa.
Hadi kamati hizo zinaunganishwa, tayari zilikuwa
zimejipambanua kama kamati zenye wajumbe waliokuwa wameonyesha uthubutu,
uzalendo na utayari wa kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa fedha na
mali ya umma. Ni kamati zilizotumia vizuri Ripoti za CAG kupambana na
uozo serikalini na mashirika ya umma na kuhakikisha hatua stahiki
zinachukuliwa dhidi ya wahusika.
Hali hiyo iliwatisha viongozi serikalini na
taasisi zake na mikakati ilifanyika chinichini ili kupunguza nguvu za
CAG na kamati hizo. Hivyo, halikuwa jambo la kushangaza Spika Makinda
alipotangaza kuunganisha kamati hizo, hatua ambayo wengi waliitafsiri
kama shinikizo kutoka katika ngazi za juu serikalini.
Tunaungana na CAG, ambaye ameonyesha utumishi
uliotukuka tangu ateuliwe, kumshauri Spika Makinda kutafakari upya
uamuzi wake huo kwa kutenganisha kamati hizo kama ilivyokuwa awali. Sisi
tunadhani kwamba uamuzi wake huo ulikuwa wa kisiasa zaidi na pengine
ulilenga kuwaondoa kitanzini vigogo mafisadi walio katika utumishi wa
umma.
0 comments: