SAM TIMBE AWAKOSOA WACHEZAJI WA BONGO KUSHINDWA KUWIKA SOKA LA KIMATAIFA

 
Kocha wa zamani Yanga, Sam Timbe amesema kukosekana kwa ushawishi na dhamira ya kufanikiwa kimataifa inayowazunguka wanasoka wengi nchini, kumeifanya Tanzania kushindwa kuwika katika soka la kimataifa.
Timbe, raia wa Uganda ambaye ni Kocha Msaidizi wa The Cranes,
alisema hayo baada ya mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani kati ya Tanzania na Uganda wiki iliyopita.
Katika mchezo huo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Uganda ilishinda bao 1-0, na hivyo kujiweka kwenye wakati mzuri wa kufuzu na kuicha Tanzania inayotakiwa kushinda angalau mabao 2-0 kwenye mechi ya marudiano.
Akizungumza na gazeti hiliwakati wa mahojiano maalumu, Timbe alisema mafanikio ya timu ya taifa hutokana na malengo binafsi ya wachezaji na klabu zao katika kusaka mafanikio.
Timbe alisema, haoni uwepo wa malengo wala kiu kwa wachezaji wa Tanzania kucheza soka la kimataifa nje ya nchi, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na mifumo mibovu ya uongozi wa klabu.
“Klabu zisipokuwa na malengo ya kufanikiwa kimataifa, hata wachezaji wake nao wanapoteza taswira hiyo na athari hiyo inazikuta pia timu za taifa,” alisema Timbe.
Timbe alisema, katika kufundisha kwake soka nchini, amebaini kuwa wanasoka wa Tanzania huridhika haraka hasa wanapocheza timu za Simba na Yanga.
“Uganda inafanya vizuri kwa sababu wachezaji wanapigana kufa na kupona kuingia timu ya Taifa na wakipewa nafasi hawafanyi makosa kwa sababu famanikio ya mchezaji yako kwenye timu ya Taifa,” aliongeza.
Kuhusu klabu, Timbe alisema klabu za Tanzania zinapaswa kulaumiwa kwa sababu ya kutokuwa na malengo na mifumo mibovu ya uongozi ndiyo maana hazifanyi vizuri nje ya Tanzania.
Akizitolea mfano klabu kubwa za Simba na Yanga, amesema zimekosa hamu ya kufanikiwa kimataifa kwa sababu mifumo yao ya uendeshaji inaangalia zaidi kushinda ligi ya nyumbani tu.
CHANZO MWANCHI
Share on Google Plus

0 comments: