''KATIBA MPYA IPENDEKEZE SIKU ZA KUFANYA IBADA'' WAJUMBE WA HALMASHAURI YA WILAYA

 
Katika Mpya imependekezwa kuwa na kipengele chenye kuzitambua siku za ibada.
Mapendekezo hayo yalitolewa na wajumbe wa mabaraza ya kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini wakati wa kikao kilichofanyika kwa siku tatu cha kuchambua na kujadili rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya mabadiliko ya katiba.
Zuberi Mjata, kutoka Kijiji cha Kwagunda Wilayani hapa, alisema kwa kuwa ibara ya 31 katika eneo la Uhuru wa Imani ya Dini inasema kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya ya imani ya dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini.
Kipengele kisemacho kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa
ni huru na jambo la hiari kwa mtu binafsi ili mradi asivunje sheria za nchi ni wazi kuwa mfanyakazi ambaye ni muumini wa dini ya Kiislamu atakapoamua kuondoka kazini siku ya ijumaa kwenda kuswaliIjumaa atakuwa anavunja sheria.
“Kwa hiyo ili kumuondoa katika hofu hiyo ni vyema katiba iwe na kifungu chenye kueleza juu ya kutambua siku za ibada na ziwe tatu badala ya mbili kama ilivyo kwa sasa,” alisema Mjata.
Mjumbe huyo alipendekeza katiba mpya iwe na kipengele chenye kutamka siku za ibada kwamba ni tatu ambazo iwe Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ili waumini wa Dini ya Kiislamu nao wakitoka kazini kwenda misikitini wasiwe ni wenye kuvunja sheria za nchi.
Ili kufidia siku ya Ijumaa mjumbe huyo alipendekeza saa za kufanya kazi ziongezeke kutoka nane za sasa hadi kufikia 10 kwa siku tano ili kufidia pengo la mapumziko ya Ijumaa.
Wajumbe wa Tume ya mabadiliko ya katiba waliopo mkoani Tanga ni Ussi.
Khamisi Haji na Riziki Shahri Mngwali ambao wameanza kupokea maoni katika Wilaya ya Korogwe na leo Jumatatu watakuwa Wilayani Muheza.
Kabla ya maoni hayo ya wajumbe wa mabaraza ya katiba, Watanzania, wamekuwa wakishiriki ibada mbalimbali katika siku za Jumapili kwa baadhi ya madhehebu ya dini, za Kikristo,  huku madhehebu mengine ya dini hiyo, yakifanya ibada zao siku ya Jumamosi na Waislamu wamekuwa wakifanya ibada za Ijumaa.
Kama pendekezo hilo litakubaliwa na baadaye kuingizwa kwenye Katiba, siku hizo za ibada zitakuwa zimetambuliwa na katiba hivyo kuzifanya ziwe za mapumziko tofauti na sasa ambapo hakuna sheria yeyote inayozitambua siku hizo kama za mapumziko. CHANZO MWANANCHI
Share on Google Plus

0 comments: