MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour
(TLP), Augustine Mrema amesema kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa
kuanzisha vikundi vya kujilinda ni sawa na kudhalilisha Jeshi la Polisi.
Ametaka jeshi hilo lisidhoofishwe kulinda raia, mali zao na amani ya
nchi kwa kuanzisha vikundi vya kufanya kazi hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
jana, ametaka vyama na wananchi kwa ujumla, washirikiane na Serikali
kuimarisha jeshi litekeleze majukumu yake.
Mrema alionya kwamba yanayotokea Misri
sasa, yanaweza kutokea nchini, ikiwa hatua za pamoja za kukabili
changamoto zilizopo katika jamii hazitachukuliwa kwani
ni rahisi
kutengeneza vikundi vitakavyogeuka vya uasi na kuleta balaa nchini.
“Hatupaswi kukosa imani na jeshi la
polisi, bado linafanya vizuri, ushahidi mzuri ni uchaguzi mdogo
uliofanyika kule Arusha hivi majuzi, amani imetawala na Polisi
walikuwepo kulinda, kwa nini tuanzishe vikundi vitakavyofanya kazi kama
polisi?” alihoji Mrema.
Hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe
kilitangaza uamuzi wa kuanzisha kambi za mafunzo ya kulinda mikutano na
viongozi wake.
Uamuzi huo wa Chadema umekosolewa siyo
tu na Polisi, bali pia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ambaye
amekionya kisithubutu kufanya hivyo akisema hatua hiyo si sahihi.
Kwa mujibu wa Tendwa, katiba ya nchi na
za vyama vya siasa, hazitakuwa na maana kama kila mwananchi au kikundi
wataruhusiwa kufanya mafunzo ya kijeshi au ukakamavu.
Sheria aliyoizungumzia Tendwa ni ya
Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inayokataza chama cha siasa kushabikia,
kutumika ama kutumia nguvu katika kufanikisha masuala yake ya kisiasa.
Kwa upande wa Msemaji wa Jeshi la
Polisi, Advera Senso, alikaririwa hivi karibuni akisema kitendo cha
chama chochote cha siasa kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume na
sheria za nchi akasema endapo watafanya hivyo, hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema polisi imeanza uchunguzi na
itachukua hatua kulingana na ushahidi utakaopatikana. Hata hivyo,
Chadema kupitia Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, kimesema
mpango wake wa kambi ya mafunzo ya kujilinda uko pale pale kwa kuwa
inafanya hivyo kwa kutumia kikundi kilicho halali kwa mujibu wa Katiba
mpya ya chama hicho ya mwaka 2006 ambayo Tendwa alikuwa mgeni wa heshima
ilipozinduliwa.
Aidha Mnyika alisema matukio ya
kushambuliwa wanachama wa chama hicho pamoja na wanataaluma wakiwemo
waandishi wa habari wanaokuwa kikazi katika shughuli za chama hicho hasa
mikutano ya hadhara, ndiyo msingi wa kuongeza ukakamavu kwa kundi lao
la brigedia nyekundu.
Mnyika akizungumzia hilo, alisema “Kwa
muda mrefu kumekuwa tukieleza kuhusu makambi ya Green Guard ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) yanayofanya mafunzo ya kijeshi…..na matukio ya
kushambuliwa kwa waandishi katika mikutano mbalimbali, ushahidi wa hayo
upo, nadhani afute kwanza kikundi cha CCM”.
Siku zilizopita, CCM iliwahi kueleza
uwepo wa kikundi chao cha vijana cha ukakamavu kilichopo tangu zamani
kwamba ni kwa ajili ya kujenga uimara wa vijana katika kukitumikia chama
na nchi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments: