POLISI mkoani Dodoma inawashikilia watu
wawili waliokuwa wakitapeli wananchi kwa kutoa vipeperushi vinavyoonesha
nafasi za kazi mbalimbali za ajira kutoka kwa kampuni inayojulikana
kama Granton Market Dubai (BJM).
Zaidi ya watu 300 mkoani Dodoma na mikoa
mingine wanadaiwa kutapeliwa katika sakata la mlolongo wa kuahidiwa
ajira; huku mmoja wao akitapeliwa Sh 400,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David
Misime, alisema kampuni hiyo haikusajiliwa na haitambuliki kisheria na
baada ya upekuzi kufanyika katika nyumba iliyotumika kama
ofisi,
zilikutwa fomu za maombi ya ajira zipatazo 320, picha ndogo za watu
mbalimbali walioomba kuajiriwa.
Aliwataja wanaoshikiliwa ni Amos Magembe
(25) mkazi wa Ipagala, Dodoma na Bariadi, mkoani Shinyanga. Mwingine ni
Shija Stanley (27) ambaye ni mkazi wa Ipagala, Dodoma na Kiloleni,
Mwanza.
Alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi
hilo uligundua kuwa kampuni hiyo haikusajiliwa na haitambuliki kisheria.
Ilidai kusaka watu kwa ajili ya nafasi 92 za ajira katika maeneo
tofauti kwa mshahara wa kati ya Sh 140,000 na 220,000 kulingana na kazi
husika.
“Tunafanya upelelezi kubaini kama
watuhumiwa hao walikuwa wakijihusisha na suala la usafirishaji haramu wa
binadamu na taarifa itatolewa baadaye,” alisema.
Kamanda Misime alisema watu hao
walikamatwa na Polisi kwa kushirikiana na wananchi. Walikamatwa katika
mtaa wa Emmaus, Kata ya Ipagala baada ya polisi kupata taarifa kutoka
kwa raia wema. Pia zilikutwa bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa
kienyeji, ikiwa ni pamoja na dawa za binadamu na manukato ya mwili.
Ilibainika kuwa ili kupata fomu ya
ajira, mwombaji alipaswa kulipia Sh 4,000 kama ada ya usajili. Kamanda
Misime alisema watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada
ya upelelezi kukamilika.
Alihadharisha wananchi juu ya watu
wanaofanya utapeli kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu akisema
vitendo hivyo vinaongezeka.CHANZO HABARI LEO
0 comments: