DAVID RUDISHA KUKOSA MASINDANO YA RIADHA NCHINI MOSCOW

epa03353379 David Lekuta Rudisha of Kenya celebrates winning the men's 800m final at the London 2012 Olympic Games Athletics, Track and Field events at the Olympic Stadium, London, Britain, 09 August 2012. At right is Nijel Amos of Botswana who placed second. EPA/BERND THISSEN +++(c) dpa - Bildfunk+++
Zambia, Zimbabwe kumenyana fainali ya Cosafa Jumamosi hii, timu za Ujerumani kujipima nguvu huko mjini Monchengladbach. David Rudhisha kukosa mashindano ya Moscow na timu za Ulaya zaanza kujianda na msimu wa ligi.
Msukosuko klabu bingwa Afrika
Mashindano ya ligi ya vilabu bingwa vya Afrika yamekumbwa na msukosuko mwishoni mwa juma hili huku mechi moja ikifutwa na nyengine ikiwa haijulikani itachezwa lini. Mkasa huo ni wa kundi B, pambano kati ya Coton Sport ya Cameroon na Sewe ya Cote dÍvoire. Pambano hilo sasa limeahirishwa kwa wiki moja pakisubiriwa matokeo ya mazungumzo baina ya chama cha kandanda cha Cameroon na Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA, kuhusu hatua yake ya kupiga marufuku shughuli zote za kandanda katika taifa hilo la Afrika magharibi.
Mchuano wa Coton na Sewe ulikuwa ufanyike Jumamosi hii huko Garoua, lakini Shirikisho la soka barani Afrika CAF limesema huenda sasa zitamenyana Julai 27 ikitarajiwa kwamba FIFA itaondoa amri yake ya kuisimamisaha Cameroon. Shirikisho hilo la soka la kimataifa liliipiga marufuku Cameroon Julai 4 kwa sababu serikali imeingilia uchaguzi wa chama cha kandanda cha nchi hiyo. FIFA sasa inataka iundwe kamati kuchunguza hali ndani ya chama hicho na kuandaa uchaguzi mpya.
Mashabiki wa timu ya zamalek wakifanya fuzo mwaka 2011.Mashabiki wa timu ya zamalek wakifanya fuzo mwaka 2011.

Zamalek, Al Ahli kucheza bila mashabiki
Pambano jengine baina ya mahasimu wawili huko Misri Zamalek na Al Ahli lililopangwa kufanyika siku ya Jumapili nalo limo hatarini. Mazungumzo yamekuwa yakifanyika kati ya chama cha soka cha Misri na na Shirikisho la kandanda barani Afrika CAF ambalo lilitaka tarehe ya mchezo huo wa Kundi A la ligi ya vilabu bingwa barani humo kibiashara ibadilishwe kwa sababu za kibiashara .
Taarifa moja kwenye mtandao iliotolewa na Al Ahlli ilisema litachezwa Jumanne au Jumatano , lakini taarifa ya Zamalek imesema ni Jumatatu au Alhamisi ijayo. Kutokana na hofu ya ukosefu wa usalama, mchezo huo utafanyika katika mji wa bandari ya sham wa El Gouna bila ya mashabiki uwanjani. Pia wakati wa kukutana miamba hiyo, utabadilishwa kwa sababu uwanja huo hauna taa za kutosha kuhudumia pambano hilo wakati wa usiku.
Zambia vs Zimbabwe fainali Cosafa

Fainali ya kombe la mataifa la Shirikisho la soka la kusini mwa Afrika Cosafa inachezwa jumamosi hii, ikiwa ni kati ya Zambia mwenyeji wa mashindano na Zimbabwe mchezo utakaofanyika. Zambia iliibwaga Afrika kusini katika pambano la nusu fainali Jumatano kwa mikwaju ya penalty mabao 5-3, baada ya kumaliza muda wa kawaida na nyongeza zikiwa bila kwa bila. Zimbabwe mabingwa watetezi wa kombe hilo nayo ikaiadhibu Lesotho mabao 2-1 katika nusu fainali nyengine. Pambano hili lla fainali kati ya Zambia na Zimbabwe katika uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, ni sawa na marudio ya ile ya 2009.
Ulaya nao wajipima nguvu

Barani Ulaya Timu kadhaa zinaendelea kujinoa kwa michuano ya kujipima nguvu kabla ya msimu wa ligi kuanza. Hapa Ujerumani mwishoni mwa Juma hili kunafanyika mashindano madogo ya timu nne ambazo ni mabingwa wa Bundesliaga na ligi ya vilabu bingwa vya ulaya na Champions league Bayern Munich, makamu bingwa wa ligi kuu ya Ujerumani na Champions league Borussia Dortmund, Wenyeji Borussia Monchengladbach na Hamburg.
Pindi ni Dortmund na Bayern zitakazochuana katika fainali Jumapili ya kesho, basi itakuwa ni marudio ya pambano la mwezi Mei la champions league ambapo Bayern waliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Dortmund hata hivyo inakabiliwa na matatizo kwani mshambuliaji wake aliyesajiliwa karibuni Henrikh Mkitaryan atakuwa nje ya chaki kwa muda wa wiki nne kutokana na maumivu ya kisigino. Lakini Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 24 na mchezaji wa kimataifa wa Armenia aliyesajili na Dortmund kwa kitita cha euro milioni 25 anatarajiwa kuwemo katika kikosi cha Dortmund kwa pambano la nyumbani dhidi ya Eintracht Braunschweig Agosti 18.
Wayne Rooney.Wayne Rooney.


Chelsea yakiri kumuwinda Wayne Rooney
Huko Uingereza harakati za usajili wa ligi kuu Premier League zinaendelea. Wiki hii kilabu ya Chelsea ilithibitisha kwamba imetuma pendekezo la maandishi kwa mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney kwa nia ya kumsajili kwa kiwango cha fedha ambacho hakikutajwa, lakini wakati huo huo ikakanusha ikisema hakuna mchezaji aliyependekezwa kwa kitita kikubwa. Akizungumza na waandishi habari mjini Bangkok-Thailand ambako Chelsea ilikuwa ziarani kwa mechi za kujipima nguvu kabla ya msimu wa ligi kuanza, Kocha wa timu hiyo Jose Morinho ambaye yumo mbioni kutafuta mshambuliaji mpya, alithibitisha kwamba kuna harakati zinazoendelea kumsajili Rooney na yaliosemwa yameshasemwa na hana la kuongeza bali wanasubiri.
Awali Morinho aliungama kwamba ana mhusudu sana Rooney. Hata hivyo Kocha wa Manchester united David Moyes amekuwa akirudi kusema mara kwa mara kwamba Rooney ambaye ametaka aruhusiwe kuihama kilabu hiyo bingwa ya England, hatouzwa. Alisema Wayne ni mchezaji wa Manu na ataendelea kuwa hivyo.
Wakati huo huo jitihada za mabingwa wa England Manchester United kutaka kumsajili, mchezaji wa kiungo wa Barcelona Cesc (the es) Fabregas zinaelekea zimegonga mwamba. Mchezaji huyo amesema hana nia yoyote ya kuihama klabu hiyo na kurejea tena England- Uingereza .
Majeraha yamuondoa David Rudisha Moscow

Mwanariadha kutoka Kenya na bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 David Rudisha hatoshiriki katika mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia mjini Moscow mwezi ujao. Rudisha alitangaza Jumanne kwamba anaendelea kupata nafuu ya goti lakini maendeleo yake ni ya taratibu, kwa hiyo kutokana na muda uliosalia hadi mashindano hayo hafikirii atakuwa amepona kikamilifu. Hayo pia yalielezwa na kocha wa mwanariadha huyo Colm O´Connell, ambaye alisikitishwa kwake akisema matumaini ya taifa la Kenya yalikuwa makubwa. Pamoja na hayo O´Connell alisema kukosekana kwa Rudisha mwenye umri wa miaka 24, katika mashindano hayo ya Moscow kutatoa nafasi kwa wanariadha wengine. Akizungumzia hilo Makamu mwenyekiti wa chama cha wanariadha nchini Kenya David Okeyo alisema wamechagua wawakilishi wenye uwezo katika mbio za mita 800 na wana uhakika hawatawangusha.
Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 David Rudisha.Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 David Rudisha.
Mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia yamepata pigo jengine kutokana na kujiondoa kwa bingwa wa dunia wa mbio za mita 100 Yohan blake wa jamaica kwa sababu ya majeraha. Mwanariadha huyo alishinda ubingwa huo katika michezo ya 2011 ya Daegu licha ya kumaliza nafasi ya pili, alipotunukiwa medali ya dhahabu kutokana na Usain Bolt pia kutoka Jamaica kuchomoka kabla ya wakati. Blake mwenye umri wa miaka 23 aliumia Aprili mwaka huu na hali hiyo ilimsababisha pia kuyakosa mashindano ya majaribio nyumbani, Jamaica.
Kutoshiriki kwake mjini Moscow mwezi ujao sio tu kutainyima Jamaica nafasi ya kumuona akitetea ubingwa wake, lakini pia Kisiwa hicho kitawakosa baadhi ya wanariadha wake ambao wamekumbwa na kashfa ya utumiaji wa madawa yaliopigwa marufuku yenye kuimarisha nguvu za misuli. Itakumbukwa Jumapili iliopita bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 100 Asafa Powell na mshindi wa medali ya dhahabu ya olimpik Sherone Simpson walisem wamegunduliwa baada ya uchunguzi kutumia aina fulani ya dawa zilizopigwa marufuku. Kashfa hiyo pia imemkumba mwanariadha wa Marekani Tyson Gay.
Katika ringi ya ubondia, Mji mkuu wa Qatar-Doha utakuwa mwenyeji wa mashindano ya ndondi ya ubingwa wa dunia, baada ya kulishinda jiji la Bangkok nchini Thailand katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka ujao 2014. Mbali na ndondi Qatar pia itakuwa mwenyeji wa Kombe la kandanda la dunia 2022 na mashindano ya ubingwa wa dunia wa mpira wa mikono-handball 2015 na ya mbio za baiskeli barabarani 2016. Uamuzi wa Jumatano wiki hii wa kuipa nafasi Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya ndondi ya ubingawa wa dunia 2015 ulichukuliwa katika mkutano wa kamati tendaji ya Chama cha kimataifa mabondia wa ridhaa mjini Jeju Korea kusini.
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani, Wolfgang Niersbach .Rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani, Wolfgang Niersbach .
Kandanda na ushoga Ujerumani
Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB limewasilisha kijigazeti kwa njia ya mtandao na kufungua mjadala kuhusu suala la Kandanda na ushoga, kwa lengo la kuwasaidia mashoga waweze kujitokeza hadharani na kujieleza jinsi walivyo. Maelezo yaliomo ni pamoja na taarifa, ufafanuzi wa maneno na anuwani za mawasiliano kuhusiana na suala hilo ambalo limekuwa ni mwiko.
Rais wa Shirikisho la kandanda la Ujerumani Wolfgang Niersbach alisema katikati ya juma kwamba kila mchezaji kandanda awe shoga wa kiume au wakike anaweza kutegemea msaada wa DFB. Waziri wa sheria wa Ujerumani Sabine Leutheusser Schnarrenberger, amependekeza kwamba kocha wa timu ya taifa Joachim loew na baadhi ya wachezaji washriki katika tamasha la kila mwaka kutetea haki za mashoga linalojulikana kama Christopher Street Day, akiongeza kwamba Shirikisho la kandanda kuwa na nafasi yake katika tamasha hilo 2014 litakuwa jambo zuri kabisa.
Mwaka 2011 mlinda mlango wa timu ya soka ya Ujerumani ya wanawake Nadine Angerer alijitokeza wazi kuungama kwamba anafanya mapenzi na watu wa jinsi zote mbili akiwataka mashoga kujitokeza bila kujali athari za kuungama kwao. Huko Marekani mchezaji mkongwe wa mpira wa vikapu Jason Collins alitangaza hadharani kupitia jarida moja amaarufu la michezo mwezi Mei mwaka huu kwamba yeye ni Shoga. Suala la Ushoga na haki za mashoga linaendelea kuwa kumzo na zingatio katika sekta mbali mbali za jamii takriban kote duniani na sasa linajikita katika sekta ya michezo.
Share on Google Plus

0 comments: