CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeshika nchi kwa
kufanya mikutano ya hadhara zaidi ya 87 mikoani ndani ya wiki moja na
kufanikiwa kupenyeza ajenda zake kwa wananchi kupitia operesheni yake ya
M4C Pamoja Daima.
Operesheni hiyo ilianza Januari 22 mwaka huu, ikiwa na lengo la kuwafikisha viongozi hao katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kupeleka ujumbe kwa umma kupitia ajenda tisa zilizopendekezwa na Kamati Kuu katika kikao chake kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.
Hii ni operesheni ambayo wadadisi wa masuala ya siasa wanasema itaisadia CHADEMA kujiimarisha na kuwapa wananchi fursa ya kujadili masuala muhimu yanayogubika taifa mwanzoni mwa mwaka 2014 baada ya misukosuko ya usaliti iliyokuwa imejitokeza.
Ajenda hizo zinazosambazwa na CHADEMA mikoani, ni mchakato wa katiba mpya katika hatua ya Bunge la Katiba, hususani suala la muundo wa serikali tatu ambalo CCM inataka kulipotosha ili liondolewe na kubakia na mfumo wa serikali mbili ambao umekuwa na kero.
Ajenda nyingine ni kura ya maoni; daftari la kudumu la wapiga kura ambapo wanakusanya orodha ya majina ya wananchi ambao wametimiza vigezo vya kujiandikisha, lakini hawajapatiwa haki hiyo ili kuishinikiza serikali iliboreshe kabla ya kura ya maoni.
Upo pia uchaguzi wa madiwani katika kata 27 ambao kampeni zake zinaendelea pamoja na ule wa jimbo la uwakilishi la Kiembe Samaki visiwani Zanzibar.
CHADEMA pia imejikita katika ujenzi wa chama ngazi za chini; uchaguzi ndani ya chama; uchaguzi serikali za mitaa na kuandaa umma kwa uchaguzi mkuu 2015.
Chama hicho ambacho kimejigawa katika vikosi sita vinavyotumia usafiri wa magari na helikopta, kimeweza kufika katika maeneo mengi nchi nzima kwa muda mfupi ikilinganishwa na ziara ya CCM mwishoni mwa mwaka jana ambapo walitumia wiki tatu katika mikoa mitatu ya Nyanda za Juu Kusini.
Ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, aliiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa usafiri wa helikopta ni nafua na wa haraka ambao unawapa fursa ya kufanya mikutano kati ya mitano hadi saba katika mkoa mmoja kwa siku.
“Kama tungekuwa tunatumia magari kwa muda wa wiki hii moja tungekuwa tumeweza kufika katika mkoa mmoja, na hivyo mkakati wetu wa kutembea nchi nzima ndani ya wiki mbili usingefanikiwa.
“Na operesheni hizi zinagharamiwa kwa asilimia kubwa na michango ya wanachama na wafadhili wetu, ruzuku ya chama pekee haitoshi, watu wanajitolea kwa hali na mali,” alisema Makene.
Katika kuanza wiki ya pili na ya mwisho ya lala salama ya operesheni hiyo, vikosi vya CHADEMA vimebadilishana maeneo jana, ambapo Mwenyekiti, Freeman Mbowe baada ya kumaliza mikoa ya Geita na Kagera ameelekea Iringa.
Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa aliyekuwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini alisafiri kuelekea mkoani Geita huku timu ya Mwanasheria wa chama, Tundu Lissu ikiendelea kufunika anga mikoa ya Kanda ya Kati.
Mkurugenzi wa habari na mawasiliano, John Mnyika na timu yake, jana waliingia mkoani Shinyanga ambako wataunganisha hadi Simiyu.
Mbowe Geita
Janet Josiah anaripoti kutoka Geita kuwa juzi Mbowe alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara na kusema kuwa serikali haina budi kuwawajibisha na kuwafikisha mahakamani maofisa wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Mbowe ambaye aliungana na Mnyika katika mkutano huo akitokea Kagera, aliwahimiza wananchi kuwaibua na kuwaweka hadharani baadhi ya maofisa wanaotumia ofisi zao kwa masilahi binafsi.
Akiwa Ngara, Bukoba mjini, Biharamulo kisha Geita, Mbowe alisema CHADEMA haiko tayari kuivumilia serikali ikiendelea kuwaacha viongozi hao pasipo kuwachukulia hatua.
Mkoani Geita, Mbowe alipokelewa kwa mabango ya kumponda aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto.
Mabango hayo yalikuwa na ujumbe mbalimbali ukiwemo ule uliosomeka “Katiba mpya ni lazima” na “CHADEMA kwanza Zitto baadaye”.
Mbowe alifafanua kuwa endapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hawatasimamia hoja za Watanzania walizozitoa katika rasimu ya pili ya katiba, CHADEMA itazunguka tena nchi nzima kuwaambia waikatae katiba katika kura za maoni.
Alisema kuwa CHADEMA itawamahasisha Watanzania wasipige kura endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitalifanyia maboresho daftari la kudumu la wapiga kura ili kuondoa watu waliokufa na kuwaongeza waliotimiza sifa za kuandikishwa.
Mnyika alisema kuwa anashangazwa kuwaona baadhi ya mafisadi wakiendelea kula maisha mitaani badala ya serikali kuwafungulia mashtaka.
Aliyataja baadhi ya makampuni hewa ambayo yametuhumiwa na maofisa wa serikali kujinufaisha kwa kutumia mikataba mibovu kuwa ni Richmond, IPTL, Net Group, Dowans, Songas na Symbion.
Lema Bukoba
Kutoka mjini Bukoba mkoani Kagera, Ashura Jumapili anaripoti kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, amewashauri wananchi kutokubali kuyumbishwa kwa dhana ya udini na ukabila.
Lema ambaye pia ni mbunge wa Arusha mjini, alisema kitendo hicho kitajenga makundi miongoni mwa jamii na hakitawaletea mabadiliko ya kimaendeleo.
Mbunge huyo alitoa ushauri huo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Bukoba ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
Alisema kuwa CCM inawachanganya na kuwayumbisha wananchi kwa itikadi za udini na kabila ili wagawanyike katika makundi iendelee kuwatawala.
Kwa mujibu wa Lema, chama chochote hakiwezi kuongoza nchi bila kupata ushirikiano wa dini zote.
Alisema chama cha siasa ni taasisi, mmoja akitoka wengine wanaendeleza taasisi hiyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Zanzibar), Said Issa Mohamed, alisema chama hicho hakina ubaguzi wa udini, ukabila wala umri.
Katika kudhihirisha hilo, aliwataja viongozi wa chama hicho ambao ni mwenyekiti Mbowe ambaye ni Mkristu Mlutheri, Dk. Slaa Mkristo Mkatoliki na yeye ambaye ni Muislamu wa dhehebu la Suni.
Lissu Dodoma
Danson Kaijage kutoka Dodoma, anaripoti kuwa Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, amewatahadharisha viongozi wa dini kuwa makini na wanasiasa ambao wanatumia fedha zao kutangaza siasa makanisani au misikitini.
Alisema kuwa wanasiasa hao wanajipenyeza katika makanisa na misikiti kwa kujifanya watoaji wazuri wa misaada wakati ni sawa na mapepo na majini yanayosambaza virusi vya udini.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini hapa juzi, Lissu alisema baadhi ya viongozi wa CCM wanajipitisha makanisani na misikitini kuomba kura, jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa kasi ya kukua kwa dhambi ya udini.
“Wapo CCM (Waislamu) wanaozungukazunguka misikitini kueneza na kuchochea virusi vya udini, ukabila na ukanda, na wapo CCM (Wakristo) wanaojikomba makanisani kueneza hayo hayo, hao si waumini wa kweli, ni majini na mapepo,” alisema na kuongeza kuwa dawa yake ni kuwafukuza kwa sababu wanaweza kusababisha dhambi ya vita ya udini.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA Taifa (BAVICHA), John Heche, alitoa siri ya chama kurusha helikopta tatu na vikosi vitatu ardhini, akisema ni kuhakikisha Watanzania wanazinduliwa wasiuzwe kama nchi ilivyouzwa kwa wageni.
“Kuna watu wanasema tunatumia fedha vibaya kurusha helikopta tatu, nauliza, tumezichukua CCM? Hapana. Tumezichukua serikalini? Hapana. Tumetoa maisha yetu, tumefanya hivyo ili tuwahi kabla Watanzania hawajauzwa kama nchi ilivyouzwa kwa wageni,” alisema.
Heche pia aligusia hatua ya Serikali ya CCM kujaribu kufanya mipango ya kutaka kukwamisha urekebishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
“Kama CCM itakuwa kichwa ngumu isiboreshe daftari hilo, tutarusha helikopta kumi angani kuzunguka nchi nzima kila kata ili kuhakikisha tunatoa elimu kwa wananchi wapige kura za kukataa mchakato wa katiba mpya,”alisema Heche.
0 comments: