MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega
mkoani Tabora, imemhukumu mkazi wa hapa kwenda jela miezi sita, kwa kosa
la utapeli wa fedha kwa njia ya mtandao wa Airtel Money kwa mawakala
mbalimbali wilayani humo.
Akitoa hukumu hiyo, Hakim Mkazi Mfawidhi,
Joseph Ngomelo, alisema mshitakiwa Helena Alexandria, atakwenda jela
miezi sita baada ya kukiri kufanya utapeli huo.
Mshitakiwa huyo alikiri kutapeli mawakala
mbalimbali wa Airtel Money waliopo Nzega mjini kwa njia ya mtandao na
kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Alisema kifungo cha mama huyo kitakuwa
fundisho kwa wanawake wangine wenye tamaa, kwani makosa kama hayo
yakiachiwa yanaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi Mkaguzi
Msaidizi, Melito Ukongoji, aliiambia Mahakama hiyo kuwa Januari mosi
mwaka 2014, mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Nzega mjini, aliiba kwa
kutumia mtandao wa Kampuni ya Airtel Money.
Alidai kuwa Hellena alikuwa akitumia ujumbe
mfupi wa maneno wenye muamala wa kutoa pesa Sh 40,000 Airtel Money na
kujipatia Sh 40,000 kwa kila wakala kwa nyakati tofauti.
Akijitetea, mshitakiwa alikiri kuhusika na
tuhuma hizo kwa nyakati tofauti na kuongeza kuwa lengo lilikuwa ni
kutafuta fedha za kujikimu kimaisha kutokana ugumu wa maisha.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo Mwendesha
Mashitaka aliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu kwa mshitakiwa huyo ili iwe
fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo za wizi wa utapeli kwa njia ya
mtandao.
0 comments: