UVCCM imesema imeunga mkono kazi zinazofanywa na sekretarieti chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na wasaidizi wake akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda, alisema Lowassa anawatumia watu kusema hovyo kupitia vyombo vya habari juu ya kazi na juhudi zinazofanywa na sekretarieti.
“Lowassa amekuwa akiwatumia watu kusema ovyo, kwanza mwenyewe hana sifa ya kuwa rais wala kuwa amiri jeshi mkuu wa nchi, na kama wapo vijana hapa mjini wanaotaka fedha kwa haraka wamtafute,” alisema.
Makonda aliongeza kuwa UVCCM wanatambua na kuthamini juhudi za katibu mkuu na sekretarieti yake katika kukijenga chama kwa kusimamia barabara misingi na shabaha ya kuundwa kwake.
Alisema kuwa inapofika wakati wasimamizi wa chama wanaanza kupigwa vita juu ya kusimamia kanuni za chama hiyo si sahihi.
“Haiwezekani matajiri na watu wenye uchu wa madaraka watake kukihodhi chama na waratibu mikakati ya kukihujumu kwa fedha zao huku sisi vijana tukitazama. Tunasema kutakilinda chama chetu na tutawalinda viongozi wetu waadilifu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Makonda alisema kuwa wanaobezwa leo kuwa wanaharibu chama ndio wameweza kurudisha imani ya wananchi kwa chama.
Kwamba imani na matumaini ambayo tayari yalishaanza kupotea na chama kuonekana si tena cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi wa nchi hii vimerejea.
Alifafanua kuwa mtu anayebeza ziara zilizofanyika na kuwaita viongozi waliozifanya kuwa ni waropokaji na wahuni, anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.
“Mhuni ni mtu mjinga, mtu wa hovyo, hana maadili, asiyependa chama. Mhuni ni mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Makonda.
0 comments: