Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu baada ya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya kuanzisha ushirikiano wa peke yao huku zikizitenga Tanzania na Burundi.
Ushirikiano ulioanzishwa na nchi hizo unahusu
maeneo ya miundombinu, biasharana viza; ushirikiano ambao umezikera nchi
za Tanzania na Burundi.
Tayari Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta imetoa msimamo bungeni
kuhusu kuchukizwa na kitendo hicho, ambacho kinaonyesha wazi kuwa
yanayofanyika siyo dalili njema kwa jumuiya hiyo.
Sitta aliliambia Bunge juzi kuwa Serikali ya
Tanzania imechukua hatua kadhaa mpaka sasa ikiwamo kutaka ufafanuzi
kutoka Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba baada ya
wiki mbili ikishapata majibu itatoa msimamo wake.
Vilevile, Sitta alisema Tanzania haitahudhuria
mikutano ya Jumuiya hiyo yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu
zimekubaliana na kuwa na msimamo wa pamoja, huku ikiwaagiza watendaji
wake kutotoa majibu ambayo yatachukuliwa kama msimamo wa nchi.
Tangu nchi ziitenge Tanzania na Burundi, yapo
maoni mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na Watanzania ikiwamo kuzishauri
nchi zilizobaguliwa kuunda umoja wao ambao utajumuisha nchi ya Jamuhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tunachukua fursa hii kutoa msimamo wetu
kuwa chokochoko zinazofanyika kuivunja jumuiya hii hatukubaliani nazo,
kwani tunaamini kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado ni muhimu kwa
wanachi mmoja mmoja, na kwa nchi wanachama.
Zipo faida nyingi ambazo nchi wanachama
zimeshaanza kupata hata kabla ya kufikia kwa shirikisho kamili. Moja ya
faida hizo ni ushirikiano wa kibiashara na kuondelwa kwa vikwazo vya
kibiashara katika nchi hizo na kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha.
Inashangaza kuona wakati nchi nyingi duniani
zikikimbilia kuungana ili kuwa na nguvu kiuchumi, sisi Afrika Mashariki
tunaaanza kugawanyika kwa sababu zisizokuwa na mashiko. Tunaamini kuwa
chokochoko hizi zinazofanyika kwa manufaa ya baadhi ya viongozi waliopo
madarakani katika nchi zilizoamua kuanzisha umoja ndani ya jumuiya,
hivyo tuzipuuze kwa kujenga hoja badala ya kukimbilia kujitoa.
Hata yale madai ya siku nyingi kuwa Tanzania
inakatalia ardhi yake kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa nchi
washirika hayana msingi na hayawezi kuwa sababu ya nchi hizo kujitenga
wala kufanya mambo ya peke yao.
Kama wahenga walivyosema umoja ni nguvu na
utengano ni udhaifu, hivyo hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo peke
yake kama kisiwa bila kuwashirikisha majirani zake wala nchi nyingine
kama washirika wa maendeleo. Litakuwa ni jambo la ajabu, kuona nchi
ambazo zimekuwa zikikaa pamoja kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali
za kuendeleza miundombinu na kupanua biashara baina yao ghafla
zinaparaganyika na kila moja kuelekea njia yake.
Tulitarajia kwamba mafunzo yaliyopatikana kutokana
na kuvunjika kwa jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977
yalitosha, kumbe bado wapo watu wenye agenda binafsi ambazo zisipokemewa
zitaathiri hata jumuiya hii ya sasa.
Tunachukua fursa hii kuwashauri marais wa nchi
zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kuacha kutanguliza maslahi yao
mbele, badala yake wafikirie maslahi ya nchi zao. Umoja huu siyo wa
viongozi waliopo madarakani. Marais waliopo sasa katika nchi za Afrika
Mashariki wataondoka, lakini Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na Tanzania
zitabaki.
0 comments: