Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja za Dk
Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka
bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge
kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye
kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema
sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema
Makinda katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk
Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge,
akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai
kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya
Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni
zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa
posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa
Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba
kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Miundombinu.
Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa
Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu
majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti,
kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya
kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya
kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly
(Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda akijibu hoja hizo jana alisema alifanya
uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni
mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo
lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.
“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza
kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha
wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na
wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa
uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika
hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na
kuongeza:
“Kamati hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na
sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na
kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri
utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha
kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu
wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti
imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya
siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.
“Lazima walete maombi na waeleze kwa nini
wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi
nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo
ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema.
0 comments: