Zikiwa zimebaki siku mbili kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuanza mtihani wa kumaliza ngazi hiyo ya elimu, Serikali imepunguza alama za ufaulu kwa mtihani huo pamoja na ule wa Kidato cha Sita.
Pia imetangaza kuwa, mtihani wa taifa wa kidato
cha nne na sita utakuwa na alama 60 za ufaulu, huku alama 40 zilizobaki
zitatokana na zile za maendeleo ya mwanafunzi shuleni (CA).
Katika mfumo huo mpya, wizara hiyo pia imefuta daraja la sifuri na badala yake kutakuwa na daraja la tano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alitangaza uamuzi huo wa Serikali jana kwa
kueleza utekelezaji wa utaratibu huo utaanza kwenye mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne mwaka huu.
“Hatua hii imechukuliwa kutokana na changamoto
zilizojitokeza kuanzia mwaka 2011. Tangu wakati huo kumekuwa na
mabadiliko mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika,” alisema Profesa
Mchome.
Alisema kuwa, alama zilizokuwa zikitumiwa awali na
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) katika kupanga matokeo hayo, kwa
kidato cha nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F= 0-34 kwa
upande wa kidato cha sita A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54,
S=40-44 na F= 0-39.
Alisema mfumo mpya, umehusisha alama za kidato cha
nne na cha sita na kuwa kuanzia sasa A=75-100, B+=60-74, B=50-59,
C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19.
“Alama A itakuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+
itakuwa ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D
ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha kabisa,”
alisema Profesa Mchome.
Alisema pia kuwa, wamebadilisha mfumo wa madaraja ambao awali kulikuwa na daraja la kwanza, la pili, la tatu, la nne na sifuri.
“Lile la sifuri tumeliondoa, badala yake kutakuwa na daraja la tano, lengo ni kuweka mlolongo mzuri zaidi,” alisema.
Alisema, alama hizo zitakuwa ni mgando (fixed grade range).
Profesa Mchome alisema kuwa, utaratibu wa sasa wa
kupanga matokeo hayo kwa madaraja, utabadilika muda wowote kuanzia sasa
na kwamba utakaokuwa ukitumika ni ule wa wastani wa alama katika ufaulu
(Grade Point Average ‘GPA’).
0 comments: