WALIOKOSA MIKOPO VYUONI SASA WAONEWA HURUMA NA SERIKALI

 Waliokosa mikopo vyuoni wahurumiwa


WANAFUNZI 1,107 wa masomo ya kipaumbele waliokosa mkopo kutokana na fomu zao za maombi kuwa na dosari, wamehurumiwa na Serikali na sasa watapata mikopo waanze chuo.
Wanafunzi watakaonufaika ni wa ualimu wa hisabati (20), ualimu wa sayansi (164), wanafunzi wa sayansi na tiba (111), uhandisi –umwagiliaji (7), ualimu (617), sayansi ya kilimo (20), uhandisi (70) na sayansi (98).
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, Serikali imeamua kutoa nafasi ya pili kwa wanafunzi hao kwa kutafuta fedha kutoka maeneo mengine tofauti na bajeti iliyokuwepo.
Kwa mujibu wa Mulugo, baada ya wanafunzi hao kushindwa kukidhi masharti kwa fomu zao kuwa na dosari, fedha za bajeti zilizokuwa zimepangwa kwa ajili yao, zilitolewa kwa wanafunzi wengine ambao hawakuwa wa kipaumbele.
“Ni kweli kosa limefanyika na Bodi (Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, HESLB)… pamoja na kuwa na haki kisheria kuhamisha fedha kwa wanafunzi wengine, walitakiwa kushauriana na Wizara kabla ya uamuzi huo ili kupata maoni ya nini kifanyike.
“Sasa tumefikia uamuzi wa kuwapa nafasi nyingine wanafunzi wenye masomo ya vipaumbele… wanatakiwa kurekebisha dosari zao wakishindwa kufanya hivyo wakati huu, hakutakuwa na huruma tena na fedha tutawapa wahitaji wengine wazingatie hili,” alisema na kuongeza kuwa majina ya wanufaika yatatangazwa na Bodi.
Mfuko wakung’utwa, mgawanyo
Akielezea namna watakavyopata fedha nje ya bajeti iliyopangwa, Mulugo alisema HESLB itatafuta Sh bilioni 2 kutoka kwenye makusanyo ya wadeni au fedha za matumizi mengine, na Wizara itatoa Sh bilioni 1.1 ili kufikisha Sh bilioni 3.1 zitakazotumiwa na wanafunzi hao.
Akifafanua mchaganuo huo, Mulugo alisema zaidi ya Sh bilioni 1.9 zitatumika kwa ajili ya chakula na malazi, Sh milioni 221.4 kwa ajili ya vitabu na viandikio, Sh milioni 686.34 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo na Sh milioni 221.4 za mahitaji maalumu ya vitivo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Asangye Bangu, alisema kutokana na bajeti iliyotengwa, wanafunzi 31,539 kati ya wanafunzi 31,647 sawa na asilimia 99.6, walitarajiwa kupatiwa mikopo.
Asilimia 83 ya wanafunzi hao kwa mujibu wa Bangu, wamedahiliwa katika kozi za kipaumbele na kati yao, asilimia 44 wamedahiliwa katika kozi ya ualimu zisizo za sayansi.
Aidha asilimia 29 wamedahiliwa katika kozi za kipaumbele za sayansi ya tiba, ualimu wa hisabati, ualimu wa sayansi, uhandisi wa mwagiliaji, uhandisi na sayansi za wanyama, wakati asilimia 17 ni wanafunzi wa kozi zingine zisizo za kipaumbele.
Bangu alisema katika mwaka wa masomo 2013/2014, Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, iliidhinisha Sh bilioni 325 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambapo Sh bilioni 306 zilitoka serikalini na Sh bilioni 19 zilitokana na marejesho ya mikopo.
Lengo la bajeti hiyo ni kukopesha wanafunzi 94,023, wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.
Vyuo kukopwa
Akielezea wapi wanafunzi hao watapata fedha za kulipa ada ya chuo, Mulugo alisema;” Katibu (Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome) anakwenda kuandikia barua vyuo viwapokee wanafunzi hao na suala la ada liwe deni kwa Serikali. “Tutalipa deni hilo katika bajeti ijayo” alisema Mulugo.
CHANZO
HABARI LEO
Share on Google Plus

0 comments: