SERIKALI ITUMIE WASANII KUPIGA VITA MADAWA YA KULEVYA



Mwigizaji Yobnesh Yussuph  ‘Batuli’ ameiomba Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo ishirikiane wasanii kupambana na dawa za kulevya nchini.
Dar es Salaam. Wiki moja tangu kuachiwa kwa dhamana wasanii waliowahi kutamba katika video nyingi za muziki wa kizazi kipya hapa nchini, ‘Video Queen’ Agnes Gerald ‘Masogange’ na mwenzake Melisa Edward walikamatwa nchini Afrika Kusini, kwa tuhuma za kukutwa na dawa zilizodhaniwa kuwa ni za kulevya, mwigizaji Yobnesh Yussuph,  ‘Batuli’ ameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ishirikiane na wasanii katika kupambana na dawa za kulevya.
Akizungumza na Mwananchi jana, Batuli alisema iwapo Serikali itadhamiria kupambana na suala hilo, inaweza kufanikiwa kama ikiwatumia wasanii, kwani wana uwezo mkubwa katika kuhamasisha vijana kuachana na dawa hizo.
Alisisitiza kwamba kwa kuwa jamii kwa sasa imekuwa na mapenzi makubwa na sanaa ya nyumbani na kupenda kusikiliza kile ambacho kinazungumzwa na wasanii, huu ni wakati muafaka wa kuwatumia wasanii na sanaa yao, katika kuwaokoa na janga hili linalopoteza nguvu kazi ya taifa kila kukicha.
Alibainisha kwamba waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni vijana, kwa hiyo ni vema wakahamasishwa na vijana wenzao wenye majina makubwa.
Aidha Batuli alisema kupanda kwa gharama za maisha kumesababisha mabinti wengi kujiingiza katika biashara hiyo ya dawa za kulevya hivyo kuhatarisha kizazi na sasa na baadae, kutokana na ukweli kuwa dawa za kulevya zina athari kubwa kwa afya.
Share on Google Plus

0 comments: