WADAU WAMTABILIA MAKUBWA MISS TANZANIA BAADA YA KUTWAA TAJI HILO JUZI


Ni Happiness Watimanywa, alitangazwa juzi kuwa mshindi wa taji hilo baada ya safari ndefu ya kuanzia ngazi ya vitongoji, mkoa na kanda.
Dar es Salaam. Juzi katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, kamati ya shindano kubwa la urembo lenye sura ya Kitaifa, linalojulikana kwa jina la Redd’s Miss Tanzania 2013, lilimtawaza Happiness Watimanywa kuwa mshindi wa taji hilo baada ya safari ndefu ya kuanzia ngazi ya vitongoji, mkoa, na kanda.
Wadau wengi wa masuala ya urembo wanamtabiri Happiness Watimanywa kwamba huenda ataifikisha mbali Tanzania katika medani ya urembo kutokana na uelewa wake na jinsi anavyoweza kujieleza kwa ufasaha, pia kutokana na upeo alionao katika masuala ya kimataifa.
Katika mahojiano na gazeti hili baada ya shindano hilo, wadau mbalimbali wa burudani wameonyesha imani na msichana huyo anayeonekana kuwa na umri mdogo lakini mwenye upeo wa hali ya juu.
Sospeter Gerald, mbunifu wa mavazi na mtaalamu wa urembo kutoka Kenya ambaye amekuwa akifuatilia historia ya Tanzania katika masuala ya urembo kwa muda mrefu ameliambia gazeti hili kwamba safari hii, wanaweza kufika mbali kutokana na mwakilishi wao kuonekana kuwa na uwezo katika kujieleza na mwonekano pia.
Naye Alice Mutalemwa, ambaye ni mwanamitindo, aliliambia gazeti hili  kwamba Hapinness, anahitaji tu kukaa na dada mwenye hekima, amwelekeze njia, kutokana na umri wake na majaribu yaliyomo kwenye tasnia, lakini kwa jinsi alivyoonekana, anaweza kufika mbali.
Kumbukumbu za masuala ya elimu ya kimataifa zinamkumbuka binti huyo mwenye umri wa miaka 19, ni mzaliwa wa familia ya Louis Roussos ya Morogoro, amewahi kusoma Laureatte International School ya Dar es Salaam, ambapo akiwa hapo, aliwahi kwenda China na Korea kusini akiwa na wanafunzi wenzake katika matamasha mbalimbali ya elimu na michezo.
Baada ya kumaliza kidato cha nne, Happy alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Strathclyde cha Uingereza anasomea digrii ya Biashara.Kipindi ambacho Happy yupo kwenye likizo ndefu, alipata wakati mgumu wa kutokuwa na kitu cha kufanya, hivyo Happy aliamua kujihusisha na masuala ya urembo na kufanikiwa kutwaa Taji la Miss Dodoma na Miss Kanda ya Kati na hatimaye kuingia kwenye kambi ya Miss Tanzania.

Share on Google Plus

0 comments: