Chama cha
Wamiliki wa Mabasi katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), leo
wanaanza mgomo kwa kutobeba abiria kupinga magari ya Noah kuruhusiwa
kubeba abiria 14 kinyume na sheria. Uamuzi
wa kuanza kwa mgomo huo ambao unatarajiwa kusababisha tatizo la usafiri
katika mikoa hiyo ulifikiwa juzi katika kikao cha wanachama wa Akiboa.
Akizungumza
na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania
(Taboa), Enea Mrutu alisema mgomo huo ni kupinga uvunjaji wa sheria
zilizowekwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)
zinazotaka magari ya Noah kubeba abiria saba.
“ Wakuu wa
Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wamewaruhusu wenye magari ya Noah
kusafirisha abiria zaidi ya 14 ingawa kisheria gari hizo zinatakiwa
kubeba abiria saba, huu ni uvunjaji wa sheria na tunaupinga,” alisema
Mrutu.
“Hapa kuna
mambo yanafanyika kienyejienyeji, tunachopinga hapa ni kuhalalishwa kwa
magari haya kubeba abiria wakati hayana leseni ya kufanya hivyo, kuna
magari yamekata leseni zote, yanalipa kodi zote kuanza TRA,halmashauri,
Sumatra na nyingine nyingi na zinabanwa, lakini kwa magari haya tunaona
wanafanya biashara bila hata kulipa kodi stahiki,” alisema.
Hivi
karibuni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alikaririwa akiwaruhusu
wenye magari ya Noah kubeba kiasi hicho cha abiria na kwenda umbali
wowote ingawa Sumatra inawataka kwenda kilometa zisizozidi 50.
Alisema hata
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kilimanjaro, Dk Abdallah Msengi (pichani)
alitoa ruksa hiyo kwa wenye Noah kufanya biashara ya kuchukua abiria.
“Viongozi
wa serikali katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuungana na wamiliki
wa magari ya Noah inatia mashaka, tunaona hapa kuna tatizo kwa viongozi
hawa,” alisema.
Alisema Taboa na Akiboa wanasikitishwa na hatua ya viongozi hao wa Serikali kupinga wazi sheria halali ya Sumatra.
Alisema
magari ya Noah hayana leseni ya biashara,lakini viongozi hao wanatoa
maagizo kuyaruhusu kufanya safari zake sehemu zozote ile bila kujali ya
umbali na idadi ya abiria.
“Hata huko
zilipotengenezwa Japan mwisho wa kubeba ni watu saba iweje hapa
Tanzania, Kuna picha inayojengeka hapa kwani hata katika kikao
kilichofanyika Juni 19, mwaka huu mkoani Kilimanjaro wenye magari haya
wamekuwa na jeuri kuliko Sumatra,” alisema Mrutu.
Mkoa wa
Arusha ni kati ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na magari mengi aina ya
Noah yanayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka na kwenda maeneo
mbalimbali ya mji huo wa kitalii.
Kabla
ya mgomo huo wanaoupanga, wamiliki hao, waliwahi kufanya mgomo wa
kusafirisha abiria kwa kile walichodai kunyanyaswa na Sumatra.
Habari na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Chanzo - Mwananchi
0 comments: