Mbunge wa
Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM - pichani), amewataka Watanzania kuwa
makini na Sheria Mpya ya Ndoa inayotarajiwa kuletwa bungeni. Mbunge
huyo amesema sheria hiyo mpya inaweza ikasababisha nchi kuongozwa na
Rais, wabunge na madiwani wanaojihusisha na vitendo vya mapenzi ya
jinsia moja (mashoga). Keissy
alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada katika mkutano wa sita wa
Chama cha...... Wabunge cha Kupambana na Ukimwi (Tapac) uliomalizika jana
mjini hapa.
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo.
Pia alipinga
hatua ya wazazi kuwapeleka watoto wao wadogo kwenye shule za bweni kwa
madai kuwa huko ndiko wanakojifunza vitendo hivyo.
“Mnashindwa kulea watoto wenu, mnawapeleka shule za bweni wakiwa na miaka mitatu ili walelewe kizungu," alisema.
Keissy
alitolea mfano mkutano mmoja uliofanyika jijini Dar es Salaam kuwa
uliwashirikisha mashoga 400, jambo alilodai ni ishara kwamba
wanaojihusisha na vitendo hivyo wanaongezeka na hivyo kuitaka serikali
kuwapiga marufuku.
Hata hivyo,
baada ya mbunge huyo kuhitimisha mchango wake, mmoja wa vijana
wanaojihusisha na ushoga, Abdillah Ally, ambaye alikuwa amealikwa na
Tapac, alisema kuwa jamii inapaswa kukubali kwamba matendo hayo
yanafanyika.
“Tunatambua
kuwa sheria haziruhusu vitendo hivi, lakini vipo na vinafanyika na
tunapata maambukizi kwa kiwango kikubwa. Tunachokitaka tusinyanyapaliwe
na jamii bali tupewe huduma ya afya ya kujikinga na maambukizi,”
alisema.
“Mathalani,
mimi hapa nina wapenzi wanaume watatu ambao nashiriki nao mapenzi, sasa
kama nimeathirika ina maana wote wale nao wamethirika,” alisema kijana
huyo.
Akifunga
mkutano huo, Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu,
aliwasihi wanasiasa wasiwabague watu wanojihusisha na vitendo vya
ushoga, usagaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema
makundi hayo yanakabiliwa na janga la maambukizi makubwa ya virusi vya
Ukimwi, hivyo wanahitaji kusaidiwa ili kuondoka katika makundi hayo
badala ya kuwahukumu.
Mwalimu
alifafanua kuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo alikuwa anatumia
dawa za kulevya lakini baada ya kupata msaada wa kiafya, ameachana na
vitendo hivyo na sasa anaendelea vizuri chini ya uangalizi.
Mkutano huo,
uliratibiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), kama wadau wakuu
ambapo waliotoa mada mbalimbali kuhusu jinsi wanavyopambana kupunguza
maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.
Naye Mbunge
wa Chambani visiwani Zanzibar, Yusuf Salam Hussein (CUF), alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imefanikiwa kupunguza maambukizi hayo
kwa wanandoa kutokana na sheria ya kuwataka wapime Ukimwi kabla ya
kufunga ndoa.
“Zanzibar
mtu hawezi kufunga ndoa kanisani kwa padre wala msikitini kwa Sheikh
ikiwa hana kibali cha Sheha ambacho kinaonesha kuwa amepima virusi vya
Ukimwi,” alisema.
habari NA SHARON SAUWA
CHANZO: NIPASHE
0 comments: