AKIKUMBUSHIA historia kali ya Mji wa Berlin
uliyogawika wakati mmoja, Rais Barack Obama amezitahadharisha Marekani
na Ulaya dhidi ya kuridhika kunakosababishwa na amani, huku akiapa
kupunguza silaha za nyuklia.
Rais Obama pia alitangaza kuwa programu yake ya udukuzi wa
mawasiliano iliyozua zogo duniani, imenusuru maisha katika pande zote za
Atlantiki. Akihutubia umati uliokusanyika katika lango kuu la
Brandenburg, Obama alisema ipo haja ya kupunguza, silaha za nyuklia za
Marekani na Urusi, ili kuondoka katika hali ya kivita inayoendelea
kuchochea kutoaminiana baina ya serikali za mataifa hayo.
Rais Barack Obama na Meya wa Berlin Claus Wowereit wakimsikiliza
Kansela Angela Merkel. Rais Barack Obama na Meya wa Berlin Claus
Wowereit wakimsikiliza Kansela Angela Merkel.
“Tunaweza tusiishi katika hofu ya maangamizi ya nyuklia, lakini
maadam silaha za nyuklia bado zinaendelea kuwepo, hatuna usalama wa
kweli,” alisema Obama wakati akihitimisha ziara ya siku tatu barani
Ulaya, ambayo ndiyo ya kwanza tangu aliposhinda muhula wa pili.
Obama anakabiliwa na migogoro ya ndani pamoja na changamoto za sera
ya kigeni, ambavyo vinamvurugia malengo yake ya muhula wa pili. Masuala
mawili – vita vikali vinavyoendelea nchini Syria, na program ya udukuzi
wa mawasiliano – vilimzonga Obama wakati wa ziara yake nchini Ujerumani,
na vile vile katika mkutano wa kundi la mataifa nane yalioendelea
kiviwanda, G8 mjini Belfast, Ireland ya Kaskazini mapema wiki hii.
Ujerumani, nchi inayolinda sana faragha, ilitaka hasa majibu kutoka
kwa Obama kuhusiana na Programu hiyo inayoendeshwa na shirika la usalama
wa taifa la Marekani NSA. Kansela Angela Merkel, alitumia mkutano wake
na Obama kwa waandishi wa habari, kutaka kuwepo na uangalifu, katika
kutathmini wasiwasi kuhusu faragha, inagwa aliepuka kukwaruzana
hadharani na rais.
“Kunahitajika kuwepo uwiano, haya ni mapambano ambayo yataendelea,”
alisema Merkel. Obama alitoa utetezi mrefu wa programu hiyo
iliyoidhinishwa na mahakama, akiielezea kama juhudi makhsusi ambayo
imesaidia kunusuru maisha. “Tunafahamu kuhusu mashambulizi yasiyopungua
50 ya kigaidi yaliyozuiwa kwa kutumia taarifa hizi, si tu nchini
Marekani, bali pia katika maeneo mengine kama hapa Ujerumani.”
Rais Obama akiwahutubia wakaazi wa Berlin, Juni 19.2013. Rais Obama
akiwahutubia wakaazi wa Berlin, Juni 19.2013. Tukio kuu la ziara ya
Obama lilikuwa hotuba ya mchana katika lango la Brandenburg, ambako
kulikuwa na ukuta wa Berlin uliyougawa mji huo kati ya mashariki na
magharibi. Obama, aliesimama nyuma ya kidirisha cha bilauri isiyopita
risasi, alizungumza kutoka upande wa mashariki wa lango hilo, eneo
ambalo enzi hizo haikuwa rahisi kwa rais wa Marekani kukanyaga.
Hotuba ya raia Obama ililinganishwa na ile maarufu ya John F. Kennedy
ya “Ich bin ein Berliner” (Mimi ni mkaazi wa Berlin), aliyoitoa miaka
50 iliyopita, na vile vile mapokezi ya kihitoria aliyoyapata Obama
mwenyewe alipowasili mjini humo akiwa mgombea wa urais mwaka 2008. Zaidi
ya watu 200,000 walifurika katika eneo la karibu na uwanja huo
kusikiliza hotuba hiyo, iliyoakisi matarajio makubwa waliokuwa nayo raia
wa Ulaya kwa mwanasiasa chipukizi wa Marekani.
Wakati huu akiwa katika mwaka wake wa tano kama rais, Obama bado
anaendelea maarufu barani Ulaya. Lakini umati uliokusanyika kumsikiliza
siku ya Jumatano ulikuwa mdogo sana ikilinganishwa na mwaka 2008. Hotuba
yake iligusia masuala kadhaa yanayotoa changamoto kwa dunia, ambapo
alitoa wito kwa mataifa ya magharibi kuwasha upya mzuka uliyoonyesha na
Berlin wakati ambapo raia wengi walikuwa wakipambana kuunganisha tena
mji huo wakati wa vita baridi.
Rais Obama na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel wakiwa katika
mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin. Rais Obama na mwenyeji wake
Kansela Angela Merkel wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari
mjini Berlin.
“Vitisho vya sasa siyo kama ilivyokuwa nusu karne iliyopita, lakini
mapambano yanaendelea,” alisema. “Na nimekuja hapa katika mji huu wa
matumaini kwa sababu mitihani ya wakati wetu inatutaka tuwe na roho ya
kupambana ambayo mji wa Berlin ulikuwa nayo nusu karne iliyopita.”
Obama alisema Marekani inaandaa mkutano mwaka 2016, kuhusu juhudi za
usalama wa silaha za nyuklia zisizo hifadhiwa vizuri duniani kote, na
kuongeza kuwa utawala wake utajitahidi kutafuta uungwaji mkono nchini
Marekani, kuridhia Mkataba wa unaopiga marufuku majaribio ya silaha za
nyuklia. Umati wa wageni waalikwa karibu 6000 walivumilia jua kali
kushangilia mapendekezo ya Obama kuhusu silaha za nyuklia, na dhamira
yake ya kuongeza mara mbili, juhudi za kufunga gereza la Guantanamo
lililoko nchini Cuba.
Obama aliondoka mjini Berlin kwa ndege yake ya Air Force One majira
ya saa nne usiku, na kuhitimisha ziara iliyodumu kwa masaa 25, katika
jiji ambalo wakati mmoja lilikuwa mahali pa hatari kati ya muungano wa
kisovieti na mataifa ya magharibi, na ambako vita baridi vilitisha mara
nyingi kuripuka katika vita vingine vya dunia. Utawala wa Kikomunisti wa
Ujerumani Mashariki ulijenga ukuta wa Berlin, ambao uliugawa mji huo
kati ya mashariki na magharibi mwaka 1961.
Wanaharakati wa Amnesty International walifanya maandamano kupinga
kuendelea kuwepo kwa gereza la Guantanamo. Wanaharakati wa Amnesty
International walifanya maandamano kupinga kuendelea kuwepo kwa gereza
la Guantanamo. Lango la Brandenburg, ambako Obama alitoa hotuba yake, ni
jengo la tao lenye njia tano, ambalo wakati mmoja lilisimama karibu na
ukuta wa Berlin. Ukuta huo ulifunguliwa Novemba mwaka 1989, na ulivunjwa
katika miezi iliyofuata, na Ujerumani iliungana tena mwaka 1990.
Mwaka 1994 rais Bill Clinton alikuwa wa kwanza kutoa hotuba kwa
Berlin iliyoungana, na kama Obama, yeye pia alizungumza katika uwanja wa
Pariser, katika upande wa mashariki wa lango hilo, akiahidi kuwa
ubalozi mpya wa Marekani ungejengwa katika upande wa pili. Ubalozi huo
ulinfunguliwa mwaka 2008.
RAIS BARACK OBAMA AACHA GUMZO MJINI BERLIN BAADA YA KIAPO CHA KUPUNGUZA SILAHA ZA NYUKLIA
About author: Unknown
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: