TAASISI ya Wanawake na Maendelea (WAMA) imetoa
msaada wa cherehani ya kudarizi kwa mjane Fatma Almasi ambaye ni mkazi
wa Ilomba jijini Mbeya. Makabidhiano ya Cherehani hiyo yalifanyika hivi
karibuni Ikulu jijini Mbeya.
Akimkabidhi cherehani hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
WAMA alisema kuwa moja ya kazi anazozifanya ni kumuinua mwanamke
kiuchumi hivyo basi alitoa cherehani hiyo ili iweze kumsaidia mjane huyo
katika.........
maisha yake.
Mama Kikwete alisema kuwa cherehani hiyo ni moja ya vyerehani
walivyovipata kutoka nchini China kwani watu wanapoomba kusaidiwa siyo
kama vitu wanavyovihitaji vipo bali nao wanatafuta sehemu mbalimbali
wakipata wanafikisha kwa wahitaji.
“Nakutakia kila la heri katika kazi zako ila usisahau kuleta mrejesho
kama kazi inaendelea au la, isije ikatokea baada ya muda cherehani
ikauzwa hiyo siyo maana yake bali ifanye kazi ya kuzalisha ili nawe
uweze kujiinua kiuchumi,” alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Fatma Almasi alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada
aliompatia kwani amekuwa akihitaji kuwa na cherehani ya kudarizi kwa
kuwa uwezo wa kudarizi anao lakini hakuwa na kitendea kazi na aliahidi
kuongeza cherehani kingine kutokana na nguvu zake mwenyewe. Fatma
alisema, “Kinamama tujitahidi kujikwamua kimaisha kwani mwanamke
akiwezeshwa anaweza,
tusiwe wategemezi kwa kina baba na mtu asijione kuwa yeye ni mjane au
anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hawezi kufanya jambo lolote na kuona
kuwa ni mwisho wa maisha bali ajitahidi kuwa mjasiriamali kwa kufanya
hivyo ataweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha”.
Aliwaomba wanawake kumuunga mkono na kumtia nguvu Mama Kikwete kwani
ana moyo wa huruma na upendo wa kuwasaidia kina mama na watoto wa kike.
Taasisi ya WAMA imekuwa ikiwainua wanawake kiuchumi, kutoa ufadhili wa
masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha
afya ya mama wajawazito na watoto na kuwasaidia watoto yatima na
wanaoishi katika mazingira hatarishi.
VIONGOZI wa Serikali, Dini na Vyama vya Siasa nchini wametakiwa
kuondoa tofauti zao na kutumia majukwaa kuhubiri amani na upendo ili
kudumisha mshikamano na utulivu ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mchungaji wa Kanisa la Moravian
Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Itiri Daniel Siame wakati
wa ibada ya mazishi ya Ditective Sagenti Christopher Kyendesya
aliyefariki Juni 19 mwaka huu wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa ajali
ya Pikipiki.
Mchungaji Siame alisema kuwa Serikali haina dini bali jamii ndiyo
inadini mbalimbali zikiwemo za Ukristo, Uislamu na Upagani na kuwaomba
viongozi hao pale wanapokutana na wananchi kuhubiri mambo yanayompendeza
Mwenyezi Mungu.
“Inawezekana kuwa ndani ya dini zetu kuna watu ambao wanamapokeo ya
dini tu na siyo kumtangaza Mwenyezi Mungu hivyo basi sisi kama viongozi
wa Serikali, Dini na Vyama vya siasa tunakazi kubwa ya kutangaza mambo
ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na amani na siyo mambo ya uchochezi”,
alisema Mchungaji Siame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alimshukuru
mchungaji huyo kwa kuwahimiza watu wote wakiwemo viongozi na wananchi
kuhusu umuhimu wa amani na upendo katika jamii.
Kandoro alisema kuwa ni jukumu lao viongozi wa Serikali, Dini na
wanasiasa kutumia lugha ya kuwajenga watanzania ili waone kuwa amani ni
silaha ya maisha yao ya kila siku kwani ikivurugika msingi mkubwa wa
maisha unaharibika na hakuna hata mmoja atakayefurahi kuona kuwa amani
na upendo vinatoweka.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa viongozi mbalimbali
waliohudhuria mazishi hayo wakiwemo pia maofisa wa Jeshi la Polisi,
wanasiasa na watendaji wa Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: