MAASKOFU WAILALAMIKIA SERIKALI ISITUMIE NGUVU KUDHIBITI VURUGU ZINAZOTOKEA NCHINI

Baadhi ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania wakiwa katika ibada hiyo.
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki nchini wameitaka Serikali kutumia njia ya mazungumzo kumaliza migogoro, badala ya kutumia jazba na nguvu. Vilevile, wamesema kuwa hawako tayari kukaa kimya huku wakiona amani na utulivu nchini ikivurugika, badala yake wataendelea kusema ili amani na utulivu viweze kurejea.
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuwataka maaskofu hao na viongozi wengine wa dini nchini kuendelea kuisaidia Serikali katika kuimarisha amani na upendo miongoni mwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha Jubilee ya miaka 25 ya uaskofu wake kwenye sherehe zilizofanyika jana katika Seminari ya Mt Peter mjini Morogoro, Askofu wa Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude, alisema meza ya mazungumzo ni lazima itumike katika kuimalisha amani na upendo wa Watanzania badala ya kutumia jazba na nguvu.
Mkude alisema kwa hivi sasa kumeibuka mivutano ya kidini na kisiasa na kutoa mfano wa vurugu zilizoibuka wilayani Sengerema mkoani Mwanza juu ya nani ana haki ya kuchinja au kutokuchinja kati ya waumini wa madhehebu ya Kikristo na Waislamu.
Pia vurugu za mikutano ya kisiasa, makanisa kuchomwa, mapadri na watumishi wengine kuuawa na kuteswa, kutupwa kwa mabomu katika mikusanyiko ya watu ikiwamo makanisa na kwamba yote hayo yangeweza kumalizwa katika meza ya mazungumzo.
Vurugu kubwa zilitokea Jumamosi iliyopita mjini Arusha baada ya mtu ambaye bado hajajulikana, kutupa bomu katika mkutano wa Chadema wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika katika viwanja vya Soweto na kuua watu wawili na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Mei 2, mwaka jana, Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi aliuawa kwa kulipuliwa na bomu na askari polisi katika vurugu zilizotokea katika eneo la Nyololo mkoani Iringa.
Februaria 18, mwaka huu, Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili, Mji Mkongwe, Zanzibar aliuawa kwa kupigwa risasi asubuhi wakati akienda kuendesha misa katika Kanisa la Mtakatifu Theresia eneo la Mtoni. Mtuhumiwa wa tukio hilo, Omar Musa Makame, anaendelea na kesi mahakamani kujibu tuhuma za mauaji. Tukio lingine ni lile la watu wawili kuuawa na polisi mjini Songea, Februari 22, mwaka jana, wakati wakizuia maandamano ya wananchi wenye hasira kali waliokuwa wakipinga mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikiana.
Hivi karibuni maaskofu hao walitoa tamko la kuitahadharisha Serikali, kudhibiti vurugu za kidini na kisiasa nchini. Walionya kuwa iwapo vurugu hizo hazitadhibitiwa huenda nchi ikaingia katika machafuko.
Awali, jana Rais Kikwete akizungumza katika hafla hiyo licha ya kumpongeza Askofu Mkude kwa utumishi wake mwema wa miaka 25 ya uaskofu wake, lakini pia alimpongeza kwa kuwa na mchango katika jitihada za maendeleo zinazofanywa na Serikali.
Alisema Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro limekuwa msaada katika kuimarisha huduma za jamii ikiwamo sekta ya elimu na afya na kwamba baadhi ya zahanati na vituo vya afya vimejengwa na kupandishwa hadhi kama Hospitali ya Mt Kizito na Turiani.
Rais Kikwete aliongeza kuwa mbali ya askofu huyo kuisaidia Serikali katika nyanja hizo, pia amekuwa akiiunga mkono katika jitihada zake za kujenga amani na upendo miongoni mwa wananchi ili taifa liweze kuwa na raia wema.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alimtaja Askofu Mkude kuwa ni kuhani asiyekuwa na mwanzo wala mwisho, kwa vile anashiriki katika ukuhani wa Yesu Kristo asiyekuwa na mwanzo wala mwisho.
Alisema mpaka kufikia umri huo katika utumishi wake amekutana na mambo mengi magumu, lakini kutokana na kumtegemea Mungu zaidi ameshinda na kwamba akawaomba waumini wa Kanisa Katoliki kuendelea kumwombea na kumpa ushirikiano ikiwa ni zawadi yao pekee.
Askofu Mkude aliteuliwa kuliongoza Jimbo Katoliki la Tanga mwaka 1988 na aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Paulo II (kwa sasa ni marehemu), mwenye heri na miaka mitano baadaye alihamishiwa katika Jimbo la Morogoro ambako amelitumikia kwa miaka 20 mpaka sasa.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz
Share on Google Plus

0 comments: