MBATIA AHAMUA KUFUNGUKA


Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia ameitaka Serikali isiishie kuivunja Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Elimu, (EMAC), na badala yake iende mbali zaidi kwa kuwachukulia hatua za kisheria wajumbe wote wa kamati hiyo. Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi alisema jana mjini Dodoma kuwa kamati hiyo inahusika moja kwa moja kuua elimu nchini kutokana na kufumbia macho ufisadi ulioruhusu kusambazwa kwa vitabu visivyo na ubora. 
“Hawa ni wahujumu uchumi wa nchi yetu; wanahusika kuididimiza elimu yetu... Inaonyesha wazi kuwa watunzi wa vitabu vile hawakutumia mitalaa. Kutokuongozwa kwa mitalaa kumesababisha vitabu vile kukosa ubora. Haiwezekani mwandishi, mhariri na mhakiki, awe mtu mmoja.” alisema.
Mbatia alisema Emac imetoa ithibati kwa vitabu vyenye maudhui yasiyo sahihi au dhaifu na ambayo hayamo kwenye mihutasari huku baadhi yao vikiwa vimeiwakilisha vibaya Bendera ya Taifa pamoja na Nembo ya Taifa kwenye baadhi ya vitabu hivyo.
Alisema miongoni mwa vitabu vilivyopitishwa na Emac havina majina ya waandishi na kwamba badala ya jina la mwandishi limewekwa jina la kampuni ya uchapishaji.
“Hakuna hata kitabu kimoja chenye wasifu wa mwandishi na karibu vitabu vyote havina wahariri wakati ni lazima kila kitabu kiwe na angalau mhariri mmoja” alisema Mbatia.
Alisema kasoro nyingine iliyopo katika vitabu hivyo ni makosa mengi ya lugha iliyotumika kuandikia ambayo ni Kiswahili, hali inayoonyesha kuwa vitabu hivyo havikupitishwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
“Aibu nyingine ipo katika maelezo ambapo eti wameandika mitalaa ya shule za awali unamwezesha mwanafunzi kukua kiuchumi, kisiasa na kijamii…na kwa wale wa shule ya msingi, wanasema mtalaa unamsaidia mwanafunzi kupata uelewa wa lugha ya Kifaransa ili aweze kupata ajira…Kweli mwanafunzi wa shule ya awali anatakiwa akue kiuchumi, kisiasa na kijamii….na hii lugha ya Kifaransa inatoka wapi katika mtalaa wa Tanzania” alihoji Mbatia.
Mbatia aliitaka Serikali vilevile iviondoe sokoni vitabu vyovyote vya kiada na ziada vyenye maudhui potofu kama inavyofanya kwa bidhaa nyingine zisizo na ubora.
“Adhabu zitolewe kwa watayarishaji na wamiliki wa vitabu duni vitakavyoingizwa shuleni kinyume na taratibu ili kuzuia matendo ya rushwa…chombo cha kupokea taarifa kutoka kwa wadau wa elimu kuhusu vitabu duni kiundwe” alisema.
Alisema endapo Serikali itapuuza na kuviacha vitabu hivyo visivyo na ubora kuendelea kutumika, ubora wa elimu utazidi kuporomoka kwa sababu wanafunzi watalazimika kutumia vitabu visivyo na ubora
Habari na  Joyce Mmasi,
Chanzo - Mwananchi
Share on Google Plus

0 comments: