Kutokana na
rasimu ya Katiba Mpya kupendekeza kufutwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu,
rasimu hiyo inapendekeza waziri yeyote mwandamizi ateuliwe kukaimu
nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa rais na makamu
wake hawapo nchini kutokana na sababu zozote zile. Mapendekezo
hayo ni tofauti na Katiba ya sasa ambayo inatamka kwamba ikiwa Rais na
Makamu wake hawapo, basi nafasi hiyo ya juu katika nchi itashikwa na
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri
Mkuu aliwekwa katika orodha ya wanaoweza kukaimu nafasi hiyo katika
marekebisho ya Katiba yaliyofanywa mwaka 2000 kupitia waraka maalumu wa
Serikali (white paper) na baadaye kupitishwa na Bunge.
Kabla ya
marekebisho hayo ya 13, Ibara ya 37(3)(a) na (b) ilikuwa ikieleza kuwa
iwapo Rais na Makamu wake hawapo nafasi hiyo ilitakiwa kushikiliwa na
Spika wa Bunge na kama hayupo basi Jaji Mkuu wa Tanzania ndiye alitakiwa
kukaimu nafasi hiyo.
Lakini
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya katika Ibara ya 73(1)(b)na (c)
inaeleza kuwa endapo Rais na Makamu wake hawatakuwapo basi nafasi hiyo
itashikiliwa na waziri mwandamizi na kama hatakuwapo basi Baraza la
Mawaziri ndilo litakalokuwa na dhamana ya kuchagua mtu wa kukaimu nafasi
hiyo.
Hata hivyo,
mtu yeyote atakayekaimu nafasi ya madaraka ya Rais, kwa namna yoyote
ile, hatakuwa na madaraka ya kuteua au kumwondoa madarakani kiongozi
yeyote yule aliyeteuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba au jambo jingine
lolote kama litakavyoainishwa na Rais katika hati ya kukasimu madaraka
yake.
“Rais
atakasimu madaraka yake kwa hati maalumu aliyotia saini yake,”
inaelekeza rasimu hiyo iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii na Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kadhalika
rasimu hiyo inaeleza kuwa endapo Baraza la Mawaziri litaona kuwa Rais
hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au akili,
linaweza kuandaa azimio la kumwomba Jaji Mkuu athibitishe kwamba Rais,
kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, hawezi kumudu kazi zake.
“Baada ya
kupokea azimio hilo, atateua bodi ya utabibu ambayo itachunguza suala
hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo,” inaelekeza rasimu hiyo.
Jaji Mkuu
baada ya kutafakari ushauri na ushahidi wa kitabibu, atampelekea Spika
hati ya kuthibitisha kwamba kutokana na maradhi ya mwili au akili, Rais
ameshindwa kumudu kazi zake, na iwapo Jaji Mkuu hatabatilisha hati hiyo
ndani ya siku saba kutokana na Rais kupata nafuu na kurejea kazini, basi
itahesabiwa kwamba kiti cha Rais kipo wazi.
Kutokana na
hali hiyo, bodi ya utabibu itakayoteuliwa kwa mujibu wa Katiba
itajumuisha watu wasiopungua watatu kutoka miongoni mwa madaktari bingwa
wanaotambuliwa na sheria inayohusu madaktari ya Tanzania.
“Endapo kiti
cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu,
kupoteza sifa za uchaguzi, kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya
mwili au akili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi
Makamu wa Rais ataapishwa na kushika madaraka ya Rais kwa muda uliobaki
katika kipindi cha miaka mitano,” inaeleza sehemu nyingine ya rasimu
hiyo.
Mawaziri Wakaazi
Pia rasimu hiyo imeelezea kuwapo kwa Mawaziri Wakaazi ambao kila Mshirika wa Muungano atateua Waziri Mkaazi atakayeratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali za Washirika na kati ya Serikali ya Mshirika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Pia rasimu hiyo imeelezea kuwapo kwa Mawaziri Wakaazi ambao kila Mshirika wa Muungano atateua Waziri Mkaazi atakayeratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali za Washirika na kati ya Serikali ya Mshirika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
“Mawaziri
Wakaazi watakuwa na ofisi zao na watafanya kazi wakiwa Makao Makuu ya
Serikali ya Muungano na pamoja na majukumu mengine watakayopangiwa na
Serikali za Washirika wa Muungano,” imeeleza ibara ya 64 ya rasimu hiyo.
Inasema
Mawaziri Wakaazi watakuwa na majukumu ya kushughulikia mambo yasiyo ya
Muungano yanayohusu ushirikiano au uhusiano wa kimataifa; na kuwa kiungo
baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za Washirika wa
Muungano na baina ya Serikali za Washirika wa Muungano.
Habari na Boniface Meena
Chanzo - Mwananchi
0 comments: