EXCLUSIVE: JUMA KASEJA AZUNGUMZA KWA MARA YA KWANZA BAADA YA KUTEMWA NA SIMBA - HAJAPEWA TAARIFA RASMI NA SIMBA....


Juma Kaseja akijifua na vijana wadogo mkoani Kigoma wanaotaka kufuata nyayo zake.
Siku moja baada ya klabu ya Simba kupitia mwenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hans Pope kuthibitisha kwamba golikipa mkongwe wa timu hiyo Juma Kaseja hatoongezewa mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo aliyoichezea kwa takribani miaka 10, leo hii mtandao huu umepata nafasi ya kuongea na Juma Kaseja kutaka kujua anazungumziaje uamuzi huo wa Simba.
Kaseja ambaye ni golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania kwa sasa yupo kwao mjini Kigoma alipoenda kupumzika baada ya kumaliza majukumu yake timu ya Taifa hivi karibuni, amezungumza na mwandishi wa mtandao huu Johnson Matinde akiwa kwao Kigoma kuhusu mustakabali wake wa soka baada ya kutemwa na Simba pamoja na mambo mengine.
Akizungumzia kuhusu suala la kutoongezewa mkataba mpya na Simba, Juma Kaseja alisema kwamba taarifa hizo yeye amezisikia kwenye vyombo vya habari kama watu wengine walivyosikia na hajapata taarifa rasmi: "Jana nikiwa natokea Tanga nilipokuwa nikapata taarifa za kuhusu masuala yangu na Simba. Klabu kupitia viongozi wake imeshaongea kuhusu suala hili na mie itafika siku nitaongelea kwa kina kuhusu jambo hili, ila kwa sasa ni kweli mimi sio mchezaji wa Simba na nisingependa kuzungumzia kuhusu wao."

Akizungumzia kuhusu mustakabali wake wa soka baada ya kuachana na Simba, Kaseja alisema: "Mimi ni mchezaji mpira, hii ndio kazi yangu hivyo nitaendelea kucheza mpira. Sasa kama unavyoniona nipo hapa kwetu nafanya mazoezi ili niwe bora kwenye kazi yangu. Mengine kuhusu ni timu gani nitachezea msimu ujao ningependa tuyaache kwa sasa, utakapofikia muda muafaka wa kuzungumzia then nitaongelea jambo hilo."

Kaseja akiwa mjini Kigoma amekuwa akijifua kwenye uwanja wa Shule ya msingi Kaluta, shule ambayo Juma Kaseja alisoma na uwanja wa shule hiyo ndio ambao alianzia career yake ya soka na ndio maana kila anapokwenda mapumzikoni nyumbani kwao Kigoma hupenda kufanya mazoezi uwanjani hapo na baadhi ya wachezaji chipukizi.
Share on Google Plus

0 comments: