TUTAANDAMANA KIKWETE AKISAINI NYONGEZA BUNGE LA KATIBA

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeazimia kuongoza maandamano kote nchini, kama Rais Jakaya Kikwete ataridhia nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Viongozi wa Tucta mkoani Dodoma walisema kitendo cha wajumbe hao kulilia nyongeza ya posho kimewagusa mno na kimelifanya shirikisho hilo kutokuwa na imani na wajumbe hao.
Hadi sasa hakujawa na majibu ya moja kwa moja kuhusu msuguano unaotokana na madai hayo.
Mwenyekiti wa Tucta wa Mkoa wa Dodoma, Dk Hamoud Ndenge, alisema shirikisho halitakubali kuona mambo yasiyofaa yanaridhiwa.
“Rais akisaini nyongeza ya posho kwa wajumbe, lazima tutaandamana ili kudai madai ya wafanyakazi ambayo tulinyamazia baada ya kuona fedha nyingi zimeelekezwa katika jambo hili muhimu (Bunge),” alisema Ndenge.
Kiongozi huyo alitofautiana na mawazo ya wengi kwamba maisha katika mji wa Dodoma ni magumu na kwamba Sh 300,000 wanazolipwa sasa ni ndogo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, maisha katika mji huu bado ni rahisi na kwa msingi huo hakuna sababu ya kuwaongezea posho.
Alisema maisha ya Dodoma hata kama wangelipwa kiasi cha chini ya kiwango wanacholipwa, wangeweza kumudu.
Kwa upande wake, Katibu wa Tucta mkoani humo, Ramadhan Mwendwa, alisema kiwango wanachodai wajumbe hao ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na umuhimu wa kitu kinachofanyika.
Mwendwa aliwataka wajumbe kutambua kwamba wametumwa na watu ambao baadhi yao hawana uwezo wa kupata hata mlo mmoja kwa siku.
Share on Google Plus

0 comments: