WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ATOA SULUHU MZOZO KATI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI WILAYANI KITETO

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka wakazi wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wanaolima kwenye Hifadhi ya Jamii ya Emboley Murtangos, waridhie amri iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa ya kuwataka waondoke kwenye eneo hilo wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa suala la wapi watakwenda.
 Pinda
“Wakazi walioko kwenye hifadhi ni lazima watii amri halali ya Mahakama ya Rufaa na waondoke katika eneo husika. Wakati mko nje, ramani iangaliwe upya na kubainisha wapi mipaka ipo na walio nje ya mipaka wasibughudhiwe,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili mjini Kiteto jana asubuhi akitokea Dodoma, alipokea taarifa fupi ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji wilayani hapa, kisha akaenda kukagua eneo husika kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kibaya.
Akitumia helikopta ya Polisi, Waziri Mkuu alikagua eneo husika na kuteremka kwenye vitongoji vya Mtanzania na Laitimi, ambako aliwapa pole wananchi waliokuwepo na kusikiliza risala katika kitongoji cha Mtanzania. Katika kitongoji hicho, watu sita waliuawa na katika kitongoji cha Laitimi, watu watatu waliuawa na kundi la wafugaji wapatao 40 -50.
“Vitendo vilivyofanyika ni uhalifu mkubwa, nimepata taabu na kujiuliza ni hasira za namna gani za watu kuamua kuua wakitoka kitongoji kimoja kwenda kingine? Hii hasira inatoka wapi? Na Kwa kosa lipi hasa,” alihoji Waziri Mkuu.
“Inaonekana ni kundi la watu ambao wameandaliwa na kujipanga, wanatoka eneo moja wanakwenda eneo jingine huku wamebeba silaha. Hapana! Hali hii haivumiliki. Mkuu wa Mkoa watu hawa ni lazima watafutwe haraka, na kila mbinu zitumike hadi wapatikane,” alisisitiza.
Aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba kuna masuala mengi yanazunguka suala zima la Hifadhi ya Embuley Murtangos, yakiwemo ya kuchelewesha usajili wa eneo husika, uamuzi wa kutengwa kwa hifadhi hiyo na kutotambulika kwa mamlaka ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999. Aliutaka uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na vijiji husika ikae na kupanga upya matumizi ya ardhi.
“Lazima mkoa na wilaya mfuatilie mihutasari ya vijiji saba iliyopitisha uamuzi huo iko wapi ili kujiridhisha kama maamuzi yaliyofanyika yalishirikisha wananchi wote,” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu na wakazi hao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa kuwaeleza wakazi hao kwamba hapa nchini hakuna ardhi ambayo haina mwenyewe.
Aliutaka Uongozi wa Mkoa kushirikiana na makamishna wa Polisi waliofika wilayani humo kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanakuwa salama.
kiteto
“Nisingependa kusikia kuna tukio jingine wakati uchunguzi ukiendelea,” alisema.
Mapema, katika taarifa yake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwillo alisema hadi kufikia Januari 13, mwaka huu watu 10 walikuwa wamepoteza maisha.
Pia alisema vibanda 60 vilichomwa moto, pikipiki sita na baiskeli 53 navyo pia vilichomwa moto.
Share on Google Plus

0 comments: