DK SLAA NA MBOWE APOKELEWA KWA MABANGO YA KUJIUZULU MKOANI KIGOMA


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa amepokewa kwa mabango katika mkutano wake wa hadhara wilayani Kakonko, Kigoma lakini akawaambia waliofanya hivyo kuwa chama chake hakitayumbishwa huku akiwataka wanaosimama na mabango kumtetea Zitto Kabwe kung’oka naye ndani ya chama.

Dk Slaa yuko mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 11 kutembelea Mikoa ya Shinyanga na Kigoma kukagua na kuimarisha uhai wa chama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwenge Kakonko, Dk Slaa alisema Chadema ni chama imara na kinaendeshwa kwa misingi ya katiba na kanuni.
“Hakuna kiongozi aliye juu ya katiba, ninawaasa wote wanaobeba mabango kujiangalia kwa kuwa ninafahamu wanatumiwa.”

Kabla ya kupokewa kwa mabango hayo, Dk Slaa aliyewasili Kakonko saa 5:11 asubuhi akitokea Wilaya ya Kahama, Shinyanga alikwenda moja kwa moja katika Kata ya Mhange ambako alifanya mkutano wa hadhara.
Dk Slaa alikumbana na mabango hayo saa 8:45 mchana msafara wake ulipowasili Kakonko Mjini ukitokea Mhange.
Wakati Dk Slaa akiingia katika uwanja wa mkutano, ulio jirani na Ofisi za CCM Wilaya ya Kakonko, kuliibuka kundi la vijana wapatao watano wakiwa na mabango mkononi na kuanza kukimbia kuyafuata magari matatu ya msafara wa Dk Slaa huku wakionyesha mabango yao. Hatua hiyo iliwafanya polisi waliokuwapo eneo hilo la mkutano kuwazuia na kuanza kuwatimua lakini mara baada ya Dk Slaa kuteremka katika gari yake na kuingia uwanjani hapo, aliomba kipaza sauti na kuwataka askari hao kuacha kuwatimua wenye mabango. “Naomba msiwaondoe waacheni waje... waruhusuni kwenye mkutano na mabango yao. Waacheni waje hapa … msiwazuie, waacheni waonyeshe mabango yao na muwaruhusu tu wapite hapa mbele, msiwapige tafadhali,” alisema Dk Slaa.
Baada ya kauli hiyo, polisi waliwaruhusu vijana hao watano ambao walibakiwa na mabango manne, moja likiwa limechanika walipokuwa wanawazuia.
Mabango hayo yaliyokuwa na maandishi ya aina moja, yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Tanzania Kigoma Kakonko bila Zitto Haiwezekani”, ‘Mhe. Slaa, Mhe. Mbowe mnatakiwa kujiuzuru mara moja” na jingine lilisomeka; “Hatupo tayari kwa kusikiliza lolote bila ya Zitto”.
Mara baada ya kupanda jukwaani Dk Slaa aliwataka tena wenye mabango kusogea karibu na jukwaa kuu alipokuwa amesimama na kuanza kuwauliza maswali vijana hao iwapo wanajua Katiba ya Chadema na kama wana kadi za chama. “Naomba niwaulize, hivi nyie wenye mabango mnaijua Katiba ya Chadema?” Walimjibu: “Hapana.” Dk Slaa akawauliza tena: “Sasa mnadai nini kwa mabango yenu kama hamjui Katiba ya Chadema?”
Mmoja wa walioshika mabango hayo alijibu: “Mtetezi wetu Zitto.”
Kutokana na hali hiyo Dk Slaa aliwauliza, atakuwa amekosea akiwakabidhi kwa Polisi kuwa siyo wanachama wa Chadema lakini wanafanya vurugu katika mkutano halali?
Share on Google Plus

0 comments: