Ndoto ya Watanzania hasa wale wasio na uwezo, wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo kutibiwa haraka na kwa gharama nafuu inaelekea kuwa ya kweli.
Ni baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
kusema kuwa sasa itaweza kupunguza wagonjwa wenye matatizo ya moyo
wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 60.
Matarajio hayo ya MNH kwa wagonjwa hao yanatokana na kupata mtambo maalumu wa kisasa utakaosaidia kufanya upasuaji wa moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH,Dk Marina Njelekela
anasema kutokana na kupatikana kwa mtambo huo wa kisasa hospitalini
hapo, wanaiomba serikali iwape fedha hasa zile ambazo imekuwa ikitumia
kuwasafirisha, kuwatibu wagonjwa wa moyo hasa nchini India na
kwingineko.
Badala yake, MNH inaomba fedha hizo ziwasilishwe
hospitalini hapo ili wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa nchini.
Anasema mtambo huo unaojulikana kwa jina la Catherization Laboratory,
ndiyo mtambo ambao wagonjwa wengi nchini walikuwa wakisafirishwa nje
kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.
Anasema mtambo huo ulioigharimu serikali Sh3.6
bilioni utasaidia katika kumchunguza mgonjwa mishipa na shinikizo ndani
ya moyo na maradhi makubwa ya kazaliwa nayo kwa lengo la kujiridhisha
kama anapaswa kufanyiwa upasuaji au kuwekewa kifaa saidizi katika moyo
wake.
Anaongeza kuwa MNH imepata uwezo wa kupatiwa
mtambo huo baada ya baadhi ya madaktari wake kupatiwa mafunzo nchini
India na Israel tangu mwaka 2008 ambapo wagonjwa 453 wenye maradhi ya
moyo wamefanyiwa upasuaji.
“Kwa sasa upasuaji wa moyo unaofanyika katika
hospitali yetu (Muhimbili0 ni sawa na ule unaofanyika katika vituo
vikubwa vya upasuaji moyo duniani kote,”anasema Dk Njelekela
Mkurugenzi huyo wa MNH anasema kuwa kupatikana
kwa mtambo huo kutasaidia serikali kuondokana na mzigo wa asilimia 70 ya
wagonjwa wa moyo wanaopata rufaa ya kwenda kutibiwa nje.
“Sambamba na asilimia 70, pia serikali
itapunguza gharama ya dola za Marekani 10,000 kwa kulipia matibabu ya
mgonjwa mmoja anaetibiwa nje ya nchi ukilinganisha na Dola 6,000 kwa
matibabu ya hapa nchini.
“Kupitia uwepo wa kituo hicho hapa Muhimbili,
uongozi wa hospitali upo katika mazungumzo na Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii ili kulipia kiasi cha dola za Marekani 6,000 badala ya dola
10,000 kwa gharama ya mgonjwa mmoja anaepatiwa rufaa ya kupeleka nje ya
nchi,” anasema Dk Njelekela .
0 comments: