MASWAHIBA WA PELE NA AZAM AKADEMI SASA WAENDA KUTETEA TAJI LAO MKOANI ARUSHA WAKIWA KAMILI

Maswahiba wa Pele; Azam Akademi wakiwa na Pele alipowatembelea Chamazi mwaka jana

MABINGWA watetezi wa Kombe la Rollingstone, michuano ya kila mwaka mjini Arusha, Azam Akademi wanatarajiwa kuondoka wiki ijayo kwenda mjini humo tayari kutetea taji lao.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga  jana  amesema kwamba, Akademi wamekuwa kwenye mazoezi makali chini ya makocha wao, Vivek Nagul, Iddi Cheche na Philipo Alando kujiandaa na michuano hiyo.
Amesema maandalizi ya vijana yamekuwa ya muda mrefu na sasa wako fiti kwenda kuendeleza utemi wao katika michuano hiyo maarufu zaidi ya vijana nchini kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kama unavyojua hii ni akademi, vijana muda wote wanakuwa chuoni wakipata mafunzo mbalimbali, wanahudumiwa vizuri na wanafanya mazoezi kila siku asubuhi na jioni kwenye Uwanja wetu wa Azam Complex, Chamazi. Hivyo nakuhakikishia wako fiti na tayari kabisa,”alisema.
Akademi ya Azam inatarajiwa kuwa moja ya vyanzo vikuu vya nyota wa soka nchini baadaye na hata Mwanasoka Bora wa zamani wa Afrika, Abedi Pele alipotembelea akademi hiyo mwaka jana aliitabiria makubwa.
Pele, aliyeongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga Chamazi, alisema akademi hiyo ni bora kuliko nyingi za Ulaya na akasema wakati utafika itakuwa inapeleka wachezaji Ulaya.
Share on Google Plus

0 comments: