ABU QATADA ASALIA UINGEREZA

Serikali ya Uingereza hatimaye imeshindwa katika dakika za mwisho kwenye kesi ya kumuondosha nchini hapa mhubiri wa dini ya kiislamu mwenye itikadi kali Abu Qatada kwenda nchini Jordan.
Abu Qatada amekuwa akitakiwa na serikali ya Jordan baada ya kupatikana na hatia ya........makosa ya ugaidi mwaka 1999.
Hili limekuwa ni anguko jingine kwa Serikali ya Uingereza hasa wizara ya mambo ya ndani, ambapo Mhubiri huyo wa dini ya Kiislamu anayetambulika kisheria kama Omary Mohammed Othman,maarufu kama Abu Qatada,ameendelea kupata kinga ya mahakama ya kusalia nchini Uingereza.
Mahakama ya rufaa mjini London,kwa pamoja imeyakataa maombi ya Waziri wa mambo ya ndani Theresa May,ambaye alipeleka kesi kwa niaba ya Serikali kuomba kumuondosha Abu Qatada ambaye alipata kinga ya mahakama ya kusalia nchini Uingereza mwaka uliopita.
Mahakama hiyo imesema kuna hatari kubwa kwa Abu Qatada kupata mateso makali iwapo atakwenda kwenye mahakama za Jordan,kulingana na makosa ya Ugaidi ambayo amekuwa akituhumiwa kuyafanya.
Licha ya Mahakama hiyo kukubali kuwa Abu Qatada ni mtu hatari sana,lakini hakuna usahidi wowote chini ya sheria za haki za binadamu zinazoruhusu kumuondosha na kumpeleka nchini Jordan.
Serikali sasa,itaibidi itunge sheria kali zitakazo iwezesha kuwaondoa nchini Uingereza watuhumiwa wa makosa ya Ugaidi bila kujali amri ya mtu yeyote jambo ambalo linaonekana kuwa gumu sasa.
Hata hivyo Wizara ya mambo ya ndani ya hapa Uingereza,Imesema huu sio mwisho wa mapambano hayo ya kisheria,kwani bado watakaa chini kutafakari na kushirikiana na Jordan kuangalia namna ya kumuondosha hapa nchini kisheria bwana Abu Qatada.
Share on Google Plus

0 comments: