Klabu ya Manchester City imetuma ofa ya paundi milioni 40 kwenda kwa klabu yaLiverpool kwa ajili ya kumnunua kiungo mshambuliaji raia wa England, Raheem Sterling.
Ofa hii inakuwa ya pili toka kwa City ambao wanaonekana kuwa wamepania katika azma yao ya kumsajili kiungo huyu ambaye ametokea kuwa moja kati ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Liverpool na timu ya taifa ya England katika siku za hivi karibuni.
Taarifa hii inakuwa sehemu nyingine katika mfululizo wa ‘filamu’ inayoendelea kati yaRaheem Sterling na Liverpool baada ya kiungo huyo kuweka wazi kuwa amegoma kusaini mkataba mpya ndani ya timu hiyo inayomilikiwa na Wamarekani, Fenway Sports Group.
Awali kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita Sterling alifanya mazungumzo yaliyorekodiwa na kituo cha BBC ambapo alifichua kuwa amegoma kusaini mkataba mpya baada ya kutoridhishwa nao huku akionekana wazi kuwa amejiandaa kuondoka.
Wakala wa mchezaji huyo naye hakusita kuweka wazi kuwa mteja wake atajiunga na moja kati ya wapinzani wakubwa wa Liverpool ambapo awali ilivumishwa kuwa Manchester United na Manchester City zingeingia vitani kusaka saini yake.
Manchester City hawakuchelewa ambapo haraka waliingia sokoni na kupeleka ofa ya paundi milioni 30 ambayo Liverpool iliikataa kabla ya kuja na ofa ya pili ambayo kama ya kwanza pia imekataliwa.
Liverpool wameweka wazi kuwa hawatasikiliza ofa yoyote ambayo iko chini ya paundi milioni 50 ambazo wao kama klabu wameweka kama thamani ya mchezaji huyo.
0 comments: