Rais aliyemaliza muda wake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemkabidhi rais mpya, Jamal Malinzi mali za TFF na amemkabidhi Sh33 milioni kwenye akaunti ya shirikisho hilo.
Akikabidhi ofisi hiyo jana, Tenga alisema fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na Dola 1,390 zipo katika akaunti za TFF hivi sasa.
Alieleza fedha hizo zimebaki baada ya kufanya
malipo ya Sh158 milioni kwa ajili ya Mkutano Mkuu na malipo ya Sh56
milioni kwa ajili matayarisho ya timu ya Taifa ya Wanawake U-20
(Tanzanite) inayokwenda Msumbiji.
“Hata hivyo, leo hii Dola 415,000 (Sh664 milioni)
zimehamishwa kutoka kwenye akaunti za Kampuni ya Bia (TBL) kwenda kwenye
akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye akaunti ya TFF
ifikapo Jumanne wiki ijayo,”alisema Tenga.
Alisema, “Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu
miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa
ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL. Malipo mengine yanayofanana na hayo
ya US $ 420,000 (Sh672 milioni) yanatarajiwa kufanyika wiki mbili
kutoka sasa.”
“Ili kujiridhisha kuwa fedha za udhamini
zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa
wadhamini kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule,”
alisema Tenga.
Alisema, “Pia nakuachia Uwanja wa Karume wenye
ukubwa wa ekari 8.8, hati yake ni namba 27206 ilitolewa Novemba mwaka
1981, nakuomba hati hii iwe ndiyo kitu cha kwanza kukikumbatia, naomba
ukikumbatie, wasije wajanja-wajanja wakakulaghai ukaiweka dhamana,”
Tenga alimwambia Malinzi.
“Kuna kiwanja kingine tumenunua Tanga mjini kina
ukubwa wa ekari 19, ukarabati wa Kituo cha Ufundi umefanywa, pamoja na
sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa Karume
kuendelea,” alisema Tenga.
Naye Rais Mpya wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza
mara baada ya makabidhiano hayo alisema, “Uchaguzi umekwisha, kama kuna
ambaye tulikwaruzana kipindi cha kampeni naomba tusameheane, makundi
hayajengi, tuachane nayo. Uwezo na nia tunayo, tushirikiane tufikishe
soka letu mbele.
“Jumatatu ya Oktoba 28 niliahidi kuwapa ofisi vyama vya Sputanza,
Tasma, Twfa na Tafca, ofisi tayari imeshapatikana
na imelipiwa mwaka mmoja maeneo ya Ilala, Cargo Stars imedhamini, baada
ya msimu mmoja TFF itabidi ihangaike nayo, pia mwishoni mwa mwezi wa nne
mwaka ujao, ofisi za TFF itabidi zihame hapa zilipo ili kupisha ujenzi
wa mradi wa kisasa.”
0 comments: