YANGA YAWATULIZA MASHABIKI WAKE BAADA YA KUTOKA SARE NA WATANI WAO WA JADI, YASEMA YAELEKEZA MASHAMBULI KWA RHINO RANGERS KESHO

 


KLABU ya Yanga imewataka mashabiki wake kuwa watulivu kutokana na matokeo ya juzi ya pambano na watani wake wa jadi, Simba, ya sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha, wachezaji wa timu hiyo nao wametakiwa kuelekeza nguvu zao katika mchezo wao dhidi ya Rhino Rangers kesho pamoja na ule wa Mgambo JKT ambao sasa utafanyika Oktoba 29, badala ya Jumamosi hii.
Kadhalika baadhi ya wanachama wameelekeza shutuma zao kwa kipa Ally Mustapha ‘Barthez’, baada ya Simba kutoka kuwa nyuma kwa mabao 3-0 kipindi cha kwanza na kusawazisha mabao yote katika mechi hiyo ya kwanza ya Ligi Kuu ya watani wa jadi ya msimu wa 2013/2014.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kiziguto alisema matokeo yaliyopatikana juzi ni dhahiri kuwa yamewakasirisha wapenzi wa klabu hiyo, lakini hata hivyo aliwataka kusahau na kujipanga kwa michezo ijayo.
Kizuguto alisema kwa sasa inatakiwa wapime uwezo wa timu yao hiyo kwa kuangalia mchezo ujao na sio kuendelea kuilaumu au kuwalaumu wachezaji wake.
Alisema wachezaji walijitahidi kuonesha uwezo wao, lakini mwishoni ule ni mpira na ambao kila kitu kinaweza kutokea kwenye mpira na ilikuwa ni lazima matokeo yapatikane.
“Najua basi ina maana kusingekuwa na ligi basi kama ndio hivyo ni watu wangekaa tu na kisha mwisho wa siku angepatikana mshindi, lakini haiwezekani ni lazima mchezo uchezwe na mshindi apatikane na ndio imekuwa hivyo kwa matokeo kuwa 3-3…huo ni mpira,” alisema Kizuguto.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa mabingwa hao watetezi wa Bara, Fred Minziro alisema timu yake imejipanga vema kwa ajili ya mchezo ujao huku akisisitiza kuwa kikosi chake kilicheza vema katika mchezo wake dhidi ya Simba isipokuwa kilipoteza mwelekeo katika kipindi cha pili.
Minziro alisema wachezaji wanatakiwa kucheza kama timu kwa kuwa inayoangaliwa ni timu ya Yanga na sio mchezaji mmoja mmoja.
“Kwa sasa kinachotakiwa ni kuja kuona mchezo wetu unaofuata na kuona ni kwa kiasi gani Yanga kama timu iko poa na kujipanga katika kuendeleza mashambulizi kwa kuwa tukishinda tutakuwa na pointi nyingi zaidi. Sasa muhimu ni kuitumia mechi ijayo kwa faida ya klabu na soka kwa ujumla,” alisema Minziro.
Jana gazeti hili lilifika katika Makao Makuu ya Yanga, Mitaa ya Twiga na Jangwani, ambako ilikuta makundi ya watu nje ya klabu hiyo wakiwa wanalalamikia matokeo ya juzi huku wakielekeza lawama zao kwa kipa Mustapha ‘Barthez’ wakimtuhumu kwa kufungwa mabao ya ‘kirahisi.’
Kwa upande wa Klabu ya Simba katika Makao Makuu yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo, hali ilionekana kuwa shwari huku kukiwa hakuna makundi ya watu.
Katika mchezo wa juzi, Yanga ndio ilianza kupata bao la kwanza lililofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 15, Hamisi akafunga mengine mawili katika dakika za 36 na 45, hivyo kikosi hicho cha Ernst Brandts kwenda mapumziko kikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Lakini kipindi cha pili, kibao kiligeuka na vijana wa Abdallah Seif ‘Kibadeni’ walisawazisha bao moja hadi jingine, yakifungwa na Betram Mwombeki dakika ya 51, Mganda Joseph Owino na Mrundi Kaze Gilbert.
Katika hatua nyingine, pambano hilo la juzi la watani wa jadi, limevuna Sh 500,727,000. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mashabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya Sh 5,000, Sh 7,000, Sh 10,000, Sh 15,000, Sh 20,000 na 30,000.
Wambura alisema tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.
“Kila klabu imepata mgawo wa shilingi 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni shilingi 76,382,084.75,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja Sh 62,555,371.69, tiketi Sh 7,309,104, gharama za mechi Sh 37,533,223.01, Kamati ya Ligi Sh 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF) Sh 18,766,611.51 na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh 14,596,253.39.
Share on Google Plus

0 comments: