Miezi kadhaa imepita sasa tangu ulipozuka mjadala mkubwa wa
kitaifa kuhusu matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka
2012. Mengi tuliyasikia na mengine hayakuwekwa bayana hadi leo.
Ila kinachojulikana kwa wengi ni kuwa matokeo hayo
yalibadilishwa, kiasi kwamba alama za ufaulu zimepanda hivyo kutoa
fursa kwa wahitimu waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tano au
hata mafunzo mengine.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji kuhusu hatua
ya uongozi wa siasa kuingilia kati utendaji wa Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta), kwa kuamrisha urekebishaji wa matokeo hayo. Je, hatua
hiyo ni sahihi? wanauliza.
Aidha, wapo wanaojiuliza kama baraza hilo lina
nguvu tena ya kusimamia na kutetea uamuzi wake. Kwa watendaji wa baraza,
bila shaka wana taratibu zao kama taasisi ya kujitathmini na kuangalia
utendaji wao wa kila siku.
Hata hivyo, mimi siamini kama Katibu Mtendaji wa
Baraza la Mitihani, Dk Joyce Ndalichako alikurupuka tu siku moja na
kuamua kubadili viwango vya ufaulu vilivyolalamikiwa na watu wengi.
Bila shaka kwa kutumia wataalamu wake, kuna
utaratibu wa kitaaluma uliotumika kutathmini mfumo wa utoaji viwango wa
zamani na hatimaye kutumia mfumo mpya.
Kama taratibu hizi zilifuatwa na zikaleta matokeo
yale tuliyoyashuhudia, kwa nini baraza lilazimishwe kubadili matokeo?
Kwa nini matokeo yale yasingechukuliwa kama changamoto ya kufanyia kazi?
Kwa nini tumechagua kupingana na ukweli ulio
dhahiri, na kulazimisha kuyaona yale tu ambayo tungependa kuyaona hata
kama hayaakisi hali halisi? Bado najiuliza hivi mwaka huu tutaendelea
kutumia mfumo mpya au ule wa zamani?
Inawezekana kuwa tukiona hali ni mbaya, tutatumia
mfumo wa zamani na pale hali itakapokuwa ahueni tena tutatumia mfumo
mpya. Sasa msimamo wetu kama Taifa ni upi katika elimu?
Jambo jingine kubwa lililoambatana na tukio hili
lilikuwa ni kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza hali mbaya ya matokeo
yale. Cha kushangaza mwaka unakatika majibu ya tume hiyo hayajawekwa
bayana. Tuliambiwa kuwa maelezo aliyotoa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Bungeni ilikuwa ripoti ya awali.
Ripoti halisi iko wapi na je, Serikali imeshaanza
kujipanga kwa ajili ya matokeo yajayo, maana muda si mrefu wanafunzi
watafanya tena mitihani ya kidato cha nne mwaka huu?
Serikali inapaswa kutambua, kuthamini na
kushirikiana kikamilifu na wadau wengine wa elimu. Kuendelea kuunda tume
bila kutoa majibu, ni kuwanyima nafasi na haki wadau wengine wa elimu
ambao nao wanaweza kuchangia kuchukua hatua stahiki za kubadili hali ya
mambo. Hakuna nchi iliyoendelea bila ya kuwekeza vilivyo katika elimu
bora. Elimu bora ni pamoja na kuwa na misingi na misimamo ambayo
haiyumbishwi na hisia za kisiasa.
0 comments: