Ni jambo la kawaida kabisa kwamba taarifa zozote kuhusu Magereza nchini mwetu hazitakosa kugusia msongamano wa wafungwa. Hali mbaya ya magereza na matatizo lukuki kutoka kwenye chombo hiki muhimu kimojawapo cha Mfumo wa Haki Jinai (criminal justice system) ya nchi hii.
Sasa hivi unaposoma makala haya, idadi ya wafungwa
Magerezani ni 34,587 (18.09.13) ambao ni mfuriko wa wafungwa uliozidi
idadi inayostahili kuwamo ndani ya Magereza kwa idadi ya 5,080.
Hivi karibuni pia Jaji Mkuu Othmani Chande wakati
akifungua mafunzo kwa mahakimu ya Haki za Binadamu alidokeza pia umuhimu
wa uharakishaji wa kusikiliza kesi za mahabusi ili kupunguza msongamano
ndani ya Magereza. Suala la msongamano wa wafungwa katika magereza
yetu ni ukiukwaji wa haki za binadamu, alisema Jaji Mkuu. Je,
tutatokaje hapo?
Hivi karibuni gazeti hili lilitoa makala
iliyobeba jina “Magereza zinapofanishwa na jehanamu” lilijaribu kuelezea
hisia za watu kwa chombo chao hiki ambacho kinapaswa kuwa ni eneo la
mafunzo bora ya urekebishwaji wa wafungwa badala yake. Kulingana na
makala hayo iliyoandikwa na Dismas Lyassa, kwa namna inavyoonekana, ni
kwamba Magereza yametumika zaidi kuwaharibu wafungwa na matokeo yake ni
kwamba wafungwa asilimia 25 ya wanaoachiliwa hurudi tena gerezani.
Ni bahati mbaya kwamba si wengi, pamoja na
wanasiasa wenyewe wanaojua nafasi ya Magereza katika kuimarisha usalama
wa raia na mali zao. Fikiria tu uwezekano siku moja wafungwa 1600
walioko sasa hivi Gereza la Ukonga wavunje gereza na kuingia mitaani,
je, jiji la Dar es Salaam litakuwa na usalama? Kwa wale wenye kumbukumbu
nzuri watakambuka mwaka 1978/9 Gereza la Ukonga, wafungwa walipovunja
gereza wakiongozwa na jambazi Nyau walivyotesa jiji la Dar es Salaam.
Kazi kubwa ya Jeshi la Magereza ni urekebishaji wa
tabia za wafungwa ili kuwawezesha kujiunga na jamii kama raia wema
mara baada ya kumaliza vifungo vyao. Kwa maana nyingine, kazi ya
Magereza ni kudhibiti urudiaji (recidivism) wa wafungwa Magerezani na
hivyo kuwafanya raia wema kuishi bila bugudha.
Ebu fikiria tena kwa mfano ule ule wa Gereza la
Ukonga; iwapo wafungwa hao watatoka gerezani kama walivyoingia bila ya
urekebishaji wowote. Wakitoka gerezani watakuwa na uwezekano wa
kushawishi wenzao wasiokuwa na kazi wajiunge na vikundi vyao ni dhahiri
kwa jinsi hiyo ungezeko la uhalifu litazidi na Magereza yatafurika kama
ilivyo sasa na pia usalama wa raia utakuwa shakani.
Tafiti zinaonyesha kwamba endapo mfungwa anaweza
kugunduliwa vishawishi vinavyo msababisha kutenda kosa (criminogenic
factors) uwezekano ni mkubwa kabisa akipata tiba ya urekebishaji
inayolenga kwenye tatizo lake anaweza kuacha uhalifu na kuwa raia mwema.
Urekebishaji huchukuliwa kama tiba ya hospitali na ni muhimu kubainisha
kwa uhakika wa tatizo ili kutoa tiba sahihi inayohusika.
Hii ndiyo kazi ambayo Jeshi letu la Magereza
inapaswa kufanya na si kazi ndogo kama inavyodhaniwa. Inataka kwanza
kuwe na utashi wa kisiasa ili kuwe na mabadiliko ya kifikra, kuwekeza
katika vitendea kazi na rasilimali watu wa kutoa hiyo taaluma ya
urekebishaji.
Dhana hii ya urekebishaji wa wafungwa ni mpya
baada ya kugundulika kwamba utaratibu uliopo wa uendeshaji wa Magereza
hausadii urekebishaji wa wafungwa. Badala yake utaratibu tulio nao
unaongeza uhalifu na husababisha msongamano ndani ya magereza kama
takwimu zetu zinavyoonyesha, urudiaji wa vifungo ni asilimia 25 na
msongamano ni zaidi ya 5,080
Kama nilivyodokeza hapo juu, taaluma hii bado ni
mpya, na inajulikana kama Mkakati wa Urekebishaji wa Wafungwa kwa
kuzingatia tishio la uhalifu alionao (Offender Risk Management and
Correctional Strategy). Kwa nchi zilizoendelea kama Canada, nchi za
Scandinavia, Uingereza, Malaysia, Singapore, Korea, Australia, New
Zealand zilikwisha anza utaratibu huu tangu mwanzoni mwa miaka ya 80.
Kwa upande wa Afrika baadhi ya nchi tayari zimekwisha anza utaratibu
huu ambazo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Namibia, Zambia, Mauritius,
Kenya, Nigeria na Ghana.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
0 comments: