Mwanasheria
Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani, amesema anaunga mkono
pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kutaka kuwapo nchini mfumo
wa Muungano wa serikali tatu. Pia ameshauri kufanyika kura ya maoni ya wananchi, hasa Zanzibar kuwauliza kama wanataka Muungano au la. Jaji Bomani alitoa msimamo huo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema
anaipongeza Tume hiyo inayoongozwa na Mwenye......
kiti wake, Jaji Joseph Warioba kwa kazi nzuri iliyoifanya hadi sasa na kwa mapendekezo mazito na mazuri waliyoyatoa kwenye Rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa Juni 3, mwaka huu.
kiti wake, Jaji Joseph Warioba kwa kazi nzuri iliyoifanya hadi sasa na kwa mapendekezo mazito na mazuri waliyoyatoa kwenye Rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa Juni 3, mwaka huu.
Jaji Bomani alisema miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo,
ni pamoja na lile linalohusu Muungano wa Tanzania na kusema:
“Nakubaliana nao moja kwa moja juu ya pendekezo la kuwa na Muungano wa
serikali tatu.”
Alisema pendekezo la kuwa na serikali tatu limekuwa likipendekezwa na
Tume zote; ikiwamo ya Jaji Farancis Nyalali mwaka 1991 na ya Jaji Robert
Kisanga mwaka 1998, zilizowahi kuundwa juu ya suala hilo.
“Tume zote hizo zimeliangalia zilivyo mpaka kufikia uamuzi huo,” alisema Jaji Bomani.
Alisema muundo wa serikali mbili uliopo ulibuniwa haraka haraka na
waasisi wa nchi mbili; Zanzibar na Tanganyika, hayati Mwalimu Julius
Nyerere na marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.
Bomani alisema historia yake fupi ilikuwa kwamba, viongozi hao wawili
walikutana mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar Januari 1964.
“Hayati Karume yeye alipendekeza nchi mbili kuungana na kuwa nchi moja
mara moja. Hayati Nyerere yeye alisita kidogo kwa kuogopa kwamba
ingeonekana Zanzibar imemezwa na Tanganyika na hivyo pengine kuelekeza
maasi Zanzibar,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:
“Hivyo alipendekeza uundwe mfumo wa muda mfupi wakati mfumo wa kudumu ukifanyiwa kazi.
Suala hili walitupiwa wanasheria serikalini walitolee mapendekezo.
Wakati huo wanasheria serikalini walikuwa Waingereza. Wao walipendekeza
uigwe mfumo wa Uingereza, ambao sura yake ilifanana sana na hali
ilivyokuwa Tanzania; yaani Tanganyika ikiwa kubwa na Zanzibar ikiwa nchi
ndogo.”
Alisema ushauri huo ulikubaliwa kama mfumo wa mpito na kwamba,
ilikubaliwa kwamba ndani ya miezi 12 iundwe tume maalum kupata maoni ya
kina juu ya mfumo wa kudumu.
“Bahati mbaya sana tume hiyo haikuundwa kwa sababu mbalimbali mpaka Tume
ya Nyalali ilipoundwa mwaka 1991,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:
“Kutokana na uzoefu tulioupata na migogoro mbalimbali mpaka sasa, mimi
binafsi naunga mkono pendekezo la Tume ya Warioba la serikali tatu.
Naamini mfumo wa namna hiyo utaweza kumaliza au kupunguza migogoro
inayojitokeza mara kwa mara hasa upande wa Zanzibar kuogopa kumezwa.”
Kwa mujibu wa Jaji Bomani, suala la Muungano ni kubwa kuliko yote katika mchakato wa Katiba mpya.
“Niliwahi kutoa ushauri, ambao bado hata ningepeda kuutoa nao ni kwamba,
ifanyike kura ya maoni wa wananchi hasa wa Zanzibar kama wanautaka
Muungano au la na kama wanautaka uwe Muungano wa mfumo gani,” alisema
Jaji Bomani.
Alisema mpaka sasa maoni ambayo yamesikika ni ya viongozi; ambayo baadhi
yakitaka Zanzibar ijitoe kwenye Muungano na mengine wa kutaka kuwapo
Muungano wa mkataba.
“Lakini ni vyema sasa katika kuutafutia suluhisho la kudumu Muungano wetu wananchi wakapewa nafasi sasa,” alisema Jaji Bomani.
Alisema suala la Muungano limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu, lakini
halijapatiwa ufumbuzi na kwamba, Tume ya Jaji Nyalali na ile ya Jaji
Kisanga kuliangalia vilivyo, ushauri wao haukufuatwa.
WOGA WA GHARAMA
Jaji Bomani alisema woga wa gharama zitakazotokana na mfumo wa serikali
tatu hauna msingi, kwani inategemea serikali hizo zinafanywa vipi na
kwamba, ipo mifano mingi ya miungano ya mifumo mbalimbali duniani.
KAMATI KUU CCM YAMCHANGANYA
Alisema msimamo wa juzi wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kidogo umemchanganya, kwani upande mmoja kuna hisia kuwa CCM haitaki
serikali tatu, wakati huo huo inataka wananchi waelimishwe vya kutosha
kabla ya kutoa maamuzi yao.
Jaji Bomani aliyataja mapendekezo mengine ya Tume, ambayo yeye binafsi
anayaafiki kuwa ni pamoja na uwakilishi sawa wa jinsia katika vyombo vya
uwakilishi.
Alisema katika pendekezo hilo kunapendekezwa kuwapo kwa wawakilishi
wawili; mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, ambao ndiwo jawabu sahihi
la suala la usawa, ambalo halina haja ya kuvifanya vyombo vya uwakilishi
kuwa vikubwa sana.
“Kwa mfano ukigeuza wilaya iwe ni jimbo la uchaguzi kwa upande wa
Tanganyika utakuwa na Bunge lisilozidi wabunge 300, ambao ni idadi nzuri
kabisa,” alisema Jaji Bomani.
TANGANYIKA ITAMKWE
Pia alisema endapo kutakuwapo na serikali tatu, ni vyema serikali hizo
zikaitwa Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya
Tanganyika.
Alisema kuziita serikali ya Tanzania Visiwani na Serikali ya Tanzania
Bara, hakupendezi hata kidogo na kuhoji sababu ya kuogopa kuita Serikali
ya Tanganyika wakati Wazanzibari wanapendelea kuiita serikali yao
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”.
Jaji Bomani alisema pendekezo lingine la Tume ya Mabadiliko ya Katiba
analokubaliana nalo moja kwa moja ni lile la kutaka watendaji wakuu wa
serikali, kama vile mawaziri, naibu mawaziri na mabalozi kuthibitishwa
na Bunge.
Alisema hilo ni jambo zuri kwani ni kinga dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka.
Kuhusu pendekezo kwamba, mawaziri kutokuwa wabunge, Jaji Bomani
alipendekeza Rais kuteua mtu yeyote anayeona anafaa ikiwa ni mbunge au
la.
Alisema kama atakuwa ni mbunge, basi ajiuzulu mara moja atakapothibitishwa kuwa waziri.
Kwa mujibu wa Jaji Bomani, jambo hilo hata Marekani, Ufaransa huwa wanalifanya.
SPIKA HASIWE NA MABWANA WAWILI
Kuhusu Spika wa Bunge, Jaji Bomani alipendekeza atokane na wabunge au
nje ya Bunge, lakini akiwa ni mbunge, basi ajiuzulu ubunge wake pindi tu
atakapoteuliwa na kuthibitishwa kuwa ndiye spika.
Alisema hilo litasaidia Spika kutokuwa na mabwana wawili wa kuwatumikia; yaani jimbo lake la uchaguzi na Uspika.
Alipendekeza Mahakama ya Muungano iwe ni moja tu; yaani Mahakama ya Juu,
ambayo alisema kazi yake itakuwa kusuluhisha migogoro kati ya nchi na
nchi, kati ya raia na nchi na juu ya masuala yote yanayohusu Muugano.
Mahakama nyingine alizopendekeza ziwapo ni Mahakama ya Rufaa, Mahakama
Kuu na Mahakama za chini yake zitakazokuwa mahakama za nchi wanachama,
siyo Muungano.
DIRA ITAJE UJAMAA NA KUJITEGEMEA
Hata hivyo, alisema kuna jambo muhimu halikushughulikiwa na Tume, ambalo ni dira ya nchi au Muungano.
Hivyo, alipendekeza Katiba iseme waziwazi kabisa kuwa: “Nchi yetu ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea.”
“Lakini katika hili lazima ieleweke kwanza nini maana ya ujamaa na
kujitegemea. Vilevile, maana ya ujamaa siyo umaskini kwani hiyo ni fikra
potofu,” alisema Jaji Bomani.
ELIMU BURE
Vilevile, alipendekeza Katiba mpya itamke wazi kuwa ni wajibu wa
serikali hasa za nchi zinazotokana na Muungano kutoa elimu ya kiwango
fulani bure, kama vile darasa la 10 na iwe ni lazima.
MATIBABU BURE
Pia alipendekeza serikali kutoa matibabu bure kwa raia wake katika shule
zake na pia Katina ionyeshe maslahi ya watu na wajibu wa serikali kwa
watu, ambayo alisema hakuyaona kwenye rasimu.
Alisema serikali haisimamii rasilimali za nchi vya kutosha, jambo ambalo limekuwa likisababisha kuingiwa kwa mikataba mibovu.
Jaji Bomani alisema moja kati ya kazi kubwa za serikali ni kuwasaidia wananchi wake na kuboresha maisha yao.
Alisema anashangazwa na maoni ya baadhi ya wanasiasa wanaotaka mfumo wa serikali tatu, huku uraia wao ukiwa wa nchi tofauti.
“Yaani wananchi wa Zanzibar wawe na uraia wao na wale wa upande wa pili
wa Muungano wawe na uraia wao. Jambo hilo halitawezekana kabisa,”
alisema Jaji Bomani.
Alishauri kupatikana muda wa kutosha kuhakikisha Watanzania wanapata
katiba yenye ubora na sifa za kutosha kuliko kukimbilia kuunda katiba
mbovu kwa kigezo tu cha uchaguzi unaokuja wa mwaka 2015.
“Rasimu hii imejitahidi sana. Huu ndiyo mwanzo mzuri tuangalie jinsi ya kulimaliza vizuri,” alisema Jaji Bomani.
Aliitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutokatishwa tamaa na kauli za
baadhi ya viongozi na kutokuwa na haraka ya kumaliza kazi yake kutokana
na shinikizo mbalimbali.
“Ipewe uhuru kamili na nyenzo za kumaliza kazi yake kikamilifu,” alisema Jaji Bomani.
Bomani anakuwa miongoni mwa viongozi wakuu waliowahi kushika madaraka makubwa nchini kutoa maoni yao juu ya rasimu ya katiba.
Wengine ambao wamekuwa wazi katika suala hili ni pamoja na Edwin Mtei,
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Gavana wa Benki
Kuu na Waziri wa Fedha, ambaye ameunga mkono serikali tatu. Mtei pia ni
muasisi wa Chadema.
Wengine waliotoa maoni yao wakipinga serikali tatu ni pamoja na Peter
Kisumo, John Malecela, na baadhi ya viongozi walioko mdarakani akiwamo
Waziri wa Ushirikiano wa Afrka Mashariki, Samuel Sitta.
Kamati Kuu ya CCM nayo imekutana na kuonyesha kuwa bado inaamini katika
Muungano wa serikali mbili, ila kama wanachama wake wataamua vinginevyo
hawatakuwa na pingamizi.
CHANZO: NIPASHE
0 comments: