BAROZI WA KENYA AKEBEHI ZIARA YA OBAMA TANZANIA



BALOZI wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso(pichani), amesema ziara ya Rais Barack Obama kwa baadhi ya mataifa ya bara la Afrika, ikiwemo Tanzania, imelenga maslahi ya Marekani. Kauli hiyo ameitoa wakati umma wa Wakenya, wakiwemo wanazuoni, ukiwa na maswali mengi, wengine wakihoji sababu zilizomfanya Rais Obama afanye ziara kwa baadhi ya mataifa ya bara hili na kushindwa kuitembelea Kenya, ambako ni asili ya baba yake mzazi.
 Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Balozi Mutiso alisema kuwa.......
taifa lake halina tatizo na ziara ya Obama, kwa kuwa imepangwa kutembelea nchi ambazo Marekani ina maslahi nazo.
Balozi Mutiso, ambaye awali alitoa mtazamo hasi juu ya Mahakama ya Kimataifa ya ICC, alisema nchi yake itawakilishwa na wajumbe watakaoteuliwa kuungana naye katika ziara hiyo ya Rais Barack Obama.



Hata hivyo alisema: “Licha ya Rais Obama kutembelea nchi kadhaa katika bara letu, ziara yake itakuwa ya manufaa kwa bara zima, kwani katika nchi hizo kutakuwa na wawakilishi wetu.

“Bara la Afrika lina nchi 54, hivyo uamuzi wa rais huyo wa kuzitembelea nchi chache unatokana na maslahi yake na nchi husika atakazozitembea" alisisitiza Mutiso.

Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa uamuzi wa Rais Obama kuiruka Kenya katika ziara yake ya bara la Afrika umesababishwa na kuvurugika kwa saikolojia ya Wakenya, huku wengine wakirejea mahusiano ya kidiplomasia baina ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa ya ICC, kesi ambayo inadaiwa kuwa na mkono wa mataifa ya Magharibi, ambayo Marekani ndiye kiranja wao mkuu.

Pamoja na Marekani kutokuwa mwanachama wa ICC, lakini nchi hiyo inatajwa kuwa na sauti pamoja na shinikizo la kuhakikisha watuhumiwa wa uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu wanafikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC.

Hata hivyo, Licha ya Rais Obama kuwa na asili iliyowazi ya taifa la Kenya, hakuna sababu rasmi zinazotajwa juu ya kushindwa kwake kuikanyaga ardhi ya nchi hiyo, ambako ndiko anakotokea baba yake mzazi pamoja na ndugu zake wengine ambao bado wako nchini humo.

Wakati Wakenya wengi wakijiuliza maswali yasiyo na majibu, wafuatialiaji wa mambo wanadai kuwa zipo taarifa kuwa uamuzi wa Rais Obama kushindwa kuitembelea Kenya katika ziara yake ya bara la Afrika, ikiwamo ile ya mara ya kwanza, pia ni mkakati wa kukwepa lawama za kisiasa ndani na nje ya taifa lake, hasa kwa nchi washirika wa mfumo wa siasa za kimagharibi.

Uchambuzi huo wa wasomi unaleta tafsiri kuwa, endapo Rais Obama angefanya ziara katika taifa la Kenya wakati akiwa mwanzoni mwa awamu ya pili ya utawala wake, ingewasaidia wapinzani wake wa kisiasa nchini Marekani kujenga hoja mapema za kumdhoofisha kisiasa pamoja na kumdhalilisha yeye na Chama chake cha Democratic.

Rais Barack Obama anatarajia kufanya ziara katika mataifa ya Senegal, Afrika Kusini na Tanzania mwishoni mwa mwezi ujao, ambapo ataambatana na mke wake, Michelle Obama.

Ziara ya Rais Obama barani Afrika imelenga kukutana na wabunge, wafanyabiashara, viongozi wa sekta za umma pamoja na vijana, ambapo kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania itakuwa nchi pekee itakayonufaika na ujio huo ambapo pia itapatiwa kiasi cha dola milioni 800 za msaada.

Rais Bill Clinton na George W Bush wote walilitembelea bara la Afrika kwa nyakati tofauti wakati wakiwa katika awamu ya pili ya uongozi wao, ambapo Rais Clinton alitembelea nchi sita, huku Bush akitembelea nchi tano, Tanzania ikiwemo.

Kwa takribani wiki nzima, vyombo vya habari nchini Kenya vimekuwa vikiendesha mada ndefu juu ya ziara ya Rais Barack Obama barani Afrika, ambapo wachangiaji wengi wa mada hizo wanaonyesha mawazo ya chuki juu ya kitendo cha Rais huyo wa Marekani kuikwepa nchi yao.




Chanzo - Mtanzania
Share on Google Plus

0 comments: