![]() |
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwaonyesha watalii bilionea kitabu chenye maelezo ya vivutio vya utalii nchini. |
Watalii bilionea 100 kutoka nchi za Ulaya na Marekani wanaotumia ndege binafsi aina ya Boeing BBJ 737 HB-11Q wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuisifia, wakisema ni moja ya urithi wa dunia unaostahili kutunzwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Watalii hao walioingia nchini Machi 28, mwaka huu
wakiongozwa na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Abercombie &
Kent, Geoffrey Kent, jana walikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu aliyefika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
kuagana nao.
Mbali na Tanzania, mabilionea hao wanaozunguka
dunia pia watatembelea nchi za Italia, Botswana, Malawi, Zambia, Uganda,
Namibia, Ethiopia na Afrika Kusini.
Kundi la kwanza la matajiri hao liliingia nchini
Machi 8, mwaka huu likifuatiwa na kundi la pili lililoingia Machi 28,
mwaka huu na kutembelea Hifadhi ya Serengeti kwa siku tatu.
“Nilifika Hifadhi ya Serengeti miaka ya sitini
nikiwa kijana mdogo, lakini nimerejea nikiwa mzee na kukuta mazingira na
uasilia wa hifadhi ukiwa vilevile,” alisema Kent.
Aliongeza: “Ni jambo linalotia faraja kwa sekta ya
uhifadhi duniani, lazima tuendelee kuhifadhi Serengeti ili kuilinda kwa
faida ya vizazi vijavyo.”
Akikabidhi zawadi ya majarida na vitu mbalimbali
vinavyotangaza vivutio vya utalii nchini, Waziri Nyalandu alisema ujio
wa watalii hao matajiri ni faraja kwa sekta ya utalii, kwani ziara yao
itajenga imani kwa wenzao ambao hawajafika nchini kutembelea vivutio vya
utalii.
“Sekta ya utalii huchangia asilimia 17 ya pato la
taifa. Lengo letu ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia asilimia 25,”
alisema Nyalandu.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na
Utalii, zaidi ya watalii milioni 1.7 walitembelea nchini mwaka jana,
huku lengo la mwaka huu likiwa watalii milioni 2.
Nyalandu alisema ili kufikia lengo hilo, Serikali
inakusudia kuhamasisha utalii wa makundi kwa kutumia ndege binafsi na
mabasi kulingana na uwezo wa watalii wenyewe.
“Utalii wa makundi umeleta faida kubwa nchini,
sasa Serikali inakusudia kufungua milango zaidi ya kuhamasisha ili wengi
waje kutembelea hifadhi zetu,” alisema Nyalandu.
Baada ya kusikia kauli ya Nyalandu, Kent aliahidi
kuwa balozi wa kutangaza Sekta ya Utalii Tanzania kwenye nchi zote za
Ulaya na Marekani.
0 comments: